0

JUMLA ya wahamiaji haramu 8,100 wamekamatwa katika maeneo mbalimbali nchini katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Novemba, mwaka huu.

Kukamatwa kwa wahamiaji hao haramu, kunatokana na maofisa wa idara ya uhamiaji na maofisa wengine wa vyombo vya ulinzi, kuimarisha doria na misako katika maeneo mbalimbali.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali, Projestus Rwegasira wakati akizungumza katika kipindi cha Tunatekeleza, kinachorushwa na Televisheni ya Taifa (TBC) kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za wizara hiyo.

Alisema maofisa wa Uhamiaji, wamekuwa wakifanya msako katika maeneo mbalimbali ikiwemo nyumba za kulala wageni, masoko na maeneo mengine kwa lengo la kudhibiti wahamiaji haramu nchini.

Akizungumzia wakimbizi kutoka katika nchi za jirani, alisema Tanzania imekuwa ikiendelea kupokea wakimbizi kutoka nchi za Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) na Burundi. Alisema hadi sasa idadi ya wakimbizi katika mikoa ya Kagera na Kigoma imefikia 270, 000.

“Watu wengi wanakimbilia Tanzania kukiwa na mapigano au matatizo katika nchi zao, nchi yetu ni kisiwa cha amani na ndio sababu ya raia wengine wanaona hapa ni mahali salama kwao,” alisema Meja Jenerali Rwegasira.

Kwa mujibu wa Meja Jenerali Rwegasira, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), zinafanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha wakimbizi wote, wanapata mahitaji ya msingi na huduma za matibabu.

Katika hatua nyingine, alisema Serikali hadi sasa imefanikiwa kufanya uhakiki na usajili wa Vitambulisho vya Taifa kwa watumishi wa umma zaidi ya 500,000 nchi nzima.

Alisema Wizara yake inaendelea na maandalizi ya kutoa vitambulisho kwa Watanzania wote walio na sifa. Alisema Serikali imeanza na usajili na uhakiki wa vitambulisho hivyo kwa watumishi wa umma na kwamba hadi sasa mwelekeo ni mzuri.

Katibu Mkuu huyo alisema serikali kupitia taasisi na vyombo vyake, vina nia ya dhati ya kuhakikisha vitambulisho hivyo vinatolewa kwa Watanzania halisi kupitia nyaraka mbalimbali, zinazothibitisha utaifa wa mtu.

“Tunajumuisha Idara ya Uhamiaji, Serikali za Mitaa na maofisa wengine ili kuhakikisha vitambulisho vya taifa vinatolewa kwa watu sahihi,” alisema.

Meja Jenerali Rwegasira alisema Watanzania wote wenye sifa wana haki ya kupata vitambulisho vya taifa bure; na kwamba serikali inafanya jitihada kwa nguvu zake zote kuhakikisha suala hilo linakamilika.

“Kila Mtanzania aliye na miaka 18 na kuendelea anastahili kupata kitambulisho cha taifa, lakini tunafanya hili kwa kuhakikisha hivi vitambulisho vinatolewa kwa Watanzania halisi...,” alisema.

Katibu Mkuu huyo aliwaonya maofisa wa idara ya Uhamiaji ambao wanatuhumiwa kupokea rushwa, kama sharti la kuwahudumia wananchi, kuacha mara moja vitendo hivyo.

Alisema kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu baadhi ya maofisa kuomba rushwa ili kuwatengezea hati za kusafiia pamoja na nyaraka nyingine. “Napenda nitumie fursa hii kuwaonya maofisa hao kwani wanahatarisha kazi zao,” alisema.

Post a Comment

 
Top