SPIKA
wa Bunge, Job Ndugai amewaapisha rasmi wabunge wanne wapya, watatu
wakiwa ni wa Kuteuliwa na Rais na mmoja aliyeshinda kwenye Uchaguzi
Mdogo wa hivi karibuni jimboni Dimani, visiwani Zanzibar.
Wabunge
hao wapya walioapishwa ni Abdallah Bulembo ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Profesa Palamagamba
Kabudi ambaye ni msomi maarufu nchini na Anne Kilango Malecela aliyekuwa
Naibu Waziri na Mbunge hadi kufikia Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Mwingine
ni Ali Juma Ali ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Dimani aliyechukua nafasi
iliyoachwa wazi baada ya kifo cha Hafidh Ally Tahir kilichotokea Novemba
mwaka 2016.
Ndugai
alianza kwa kumuapisha kwanza Bulembo, akifuatiwa na Kilango, Profesa
Kabudi na baadaye Ali ambao wote kwa pamoja baada ya kula kiapo hicho,
walisalimiana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Kiongozi wa Upinzani
Bungeni, Freeman Mbowe.
Wakati
wa uapisho huo, hali ya Bunge hilo ilitawaliwa na shamrashamra na
vigelegele kutoka kwa wabunge waliokuwa wanawasindikiza wabunge hao
wapya kuingia ukumbini kwa ajili ya kuapishwa.