Askari Polisi wakiwatawanya wananchi kwenye maeneo ya stendi ya zamani Mjini Geita ambao walikusanyika kusalimiana na Waziri mkuu mstaafu ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu Taifa ya Chadema Edward Lowassa
Waziri mkuu mstaafu ambaye pia ni mjumbe
wa kamati kuu Taifa ya chama cha demokrasia na Maendeleo( Chadema)
Edward Lowassa,akiwapungia mkono wananchi wa Geita akiashiria
kuwasalimia wakati alipokuwa akipita kuelekea kata ya Nkome
Msafara wa Waziri mkuu mstaafu ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu Taifa
ya Chama cha demokrasia na Maendeleo Chadema Edward Lowassa ukipita
katika viunga vya mji wa Geita huku ukiwa umepokelewa na waendesha
pikipiki maarufu kwa jina la boda boda
Kamanda wa polisi wilaya ya Geita (OCD) Ally Kitumbo akiwatawanya wananchi ambao walikusanyika kwenye eneo la stendi ya zamani
Msafara wa Waziri mkuu mstaafu ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu Taifa Chadema Edward Lowasa ukielekea kituo cha polisi.
Baadhi ya askari wakiwa katika majukumu yao ya kikazi.
Askari wakiwa wameweka ulinzi kwenye uzio wa ngome ya makao makuu ya
jeshi la polisi mkoani Geita,ambapo kulikuwa kukifanyika mahojiano ya
Mhe Lowassa na jeshi hilo.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Geita,Mponjoli Mwabulambo akikanusha
taarifa ya kukamatwa kwa ,Waziri mkuu mstaafu ambaye pia ni mjumbe wa
kamati kuu Taifa ya chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Edward
Lowassa.
*****
Waziri mkuu mstaafu ambaye pia ni mjumbe wa kamati kuu Taifa ya Chama
Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)Edward Lowassa, pamoja na ujumbe
aliokuwa ameambatana nao wameshikiliwa na jeshi la polisi Mkoani Geita
kwa mahojiano ambayo yamedumu kwa zaidi ya masaa matat.
Tukio hilo limetoka wakati Lowassa akitokea mkoani Kagera ambapo alifika
kwenye stendi ya mabasi ya zamani kwa lengo la kusalimiana na wananchi
wakati akipita kuelekea kwenye kampeni za uchaguzi mdogo kata ya Nkome.
Tukio la kukamatwa kwa waziri mkuu huyo,lililoambatana na vipigo kwa
waandishi wa habari wawili,Valence Robert wa Channel Ten na Joel Maduka
wa Storm Fm ambaye pia ni mmiliki wa mtandao wa Madukaonline blog
limetokea leo Jumatatu Januari 16,2017 majira ya saa 9:30alasiri eneo la
stendi ya zamani ya mabasi iliyopo katika kata ya Kalangalala mjini
Geita.
Lowassa ambaye alikuwa kwenye gari yenye namba T 771 DEA aina ya V8
Land cruser na wenzake ambao ni Khamis Mgeja pamoja na Profesa Balegu
walikuwa wakitokea mjini Bukoba kuelekea mjini Geita kwenye kampeni za
uchaguzi mdogo wa udiwani unaofanyika katika kata ya Nkome wilaya ya
Geita vijijini.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo wamesema chanzo cha Lowassa
kukamatwa kilitokana na yeye kusimama kisha kuzungumza na wananchi
waliokuwa wamekusanyika katika stendi hiyo na kumweleza changamoto
zinazowakabili ikiwemo ugumu wa maisha na ukame kukithiri hali ambayo
imesabauisha baadhi ya maeneo kukumbwa na njaa.
Hata hivyo kabla ya Lowassa kuanza kujibu kilio cha wananchi ha
,kamanda wa polisi wilaya ya Geita (OCD)Ally Kitumbo alifika eneo hilo
akiwa ameongozana na askari zaidi ya kumi waliokuwa na silaha za moto
kisha kumwamuru Lowassa kwenda kituo cha polisi bila shuruti.
Kutokana na hali hiyo baadhi ya wananchi waliamua kuandamana
wakifuatilia kwa nyuma msafara wa waziri mkuu huyo mstaafu hadi kituo
kikuu cha polisi wilaya ambako ghafla yalianza kufyatuliwa mabomu ya
machozi kuwatawanya wananchi ambao wakati huo walikwishaanza kujazana
nje ya kituo hicho cha polisi kufuatilia kukamatwa kwa Lowassa.
Wakiwa katika kituo cha Polisi wilaya na baada ya kuhakikisha wananchi
wamekimbia kuokoa maisha yao ,baadaye msafara wa waziri mkuu huyo
mstaafu aliyekuwa ameongozana na Profesa Balegu na Khamis Mgeja
uliondoka kituoni hapo kuelekea makao makuu ya polisi mkoa wa Geita
ukiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi.
Hata hivyo mbali na polisi kurusha mabomu ya machozi na kupiga risasi za
moto kuwatawanya wananchi hao,waandishi wa habari wawili Valence Robert
na Joel Maduka waliokuwa eneo hilo wakitekeleza majukumu yao ya kazi
,walikamatwa kisha kuanza kushushiwa kipigo na polisi huku Maduka
akiumizwa sehemu za mgongoni wakati Robert akipigwa kwa mateke sehemu
mbalimbali za mwili wake ikiwemo kichwani,mgongoni na miguuni.
Maduka na Robert waliokolewa na OCD Kitumbo aliyefika eneo ambalo
walikuwa wakipokea kipigo kisha kuwazuia askari wake wasiendelee
kuwashambulia waandishi hao ambao kwa wakati huo walikwishakamatwa
Tanganyika jeki wakilazimishwa kuingia kituoni ili wawekwe mahabusu.
Waandishi hao walidai kuwa kitendo walichofanyiwa na polisi hao ni cha
kinyama na hakikubaliki kwa vile kinavunja haki za binadamu ikizingatiwa
kuwa walikuwa wakitekeleza majukumu yao bila kuvunja sheria za nchi.
"Kwa kweli nimeumizwa sana sehemu za mgongoni lakini pia kitendea kazi
changu ambayo ni kamera ilirushwa kwa minajili ya kuivunja lakini
kutokana na ugumu wa kifaa changu hakikuweza kudhurika sasa najiuliza
hivi hii ni haki na je Tanzania kuna uhuru wa vyombo vya habari maana
kama mwandishi anavamiwa eneo lake la kazi kisha kupigwa bila
sababu’’,alisema Maduka.
Kwa upande wake Robert ambaye kwa sasa anachechemea kutokana na maumivu
aliyoyapata kutokana na kipigo hicho alidai amesikitishwa na kitendo cha
polisi kuvunja kamera yake ambayo amekuwa akiitumia kutekeleza majukumu
yake na hajui iwapo jeshi hilo litamlipa au la.
Kwa mujibu wa waandishi hao wamedai wamepanga kuchukua PF3 kisha
kufungua kesi mahakamani ili kudai haki zao kutokana na kitendo cha
udhalilishaji walichofanyiwa.
Aidha Mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Geita(GPC)
Daniel Limbe mbali na kulaani kitendo hicho ameelekeza kwa waandishi
waliokumbwa na madhila hayo kuhakikisha wanapata PF3 ili baadaye uongozi
wa GPC umwandae wakili wake ambaye atasimamia kesi hiyo mahakamani.
"Nimesikitishwa na kitendo walichofanyiwa waandishi hao na nimeelekeza
wahakikishe wanachukua PF3 ya matibabu ili tumwandae wakili wetu ambaye
atasimamia kesi hiyo itakapofikishwa mahakamani lengo ni kuonyesha
kukerwa na vitendo vya polisi vya kuwakamata na kuwapiga waandishi bila
sababu wanapotekeleza wajibu wao wa kihabari’’,alisema Limbe.
Kamanda wa polisi mkoa wa Geita Mponjoli Mwabulambo amekanusha taarifa
ya kukamatwa kwa Lowassa na kwamba walimzuia kwa ajili ya usalama na
masuala mengi ambayo wamezungumzia ni jambo la ulinzi na kwamba
walilenga katika suala la ulinzi wa jamii na usalama wa wao wenyewe.
“Kiswahili kizuri kwamba tulikuwa tumemzuia hatukuwa tumemkata isipokuwa
tulikuwa tumemzuia ule msafara wake kwa ujumla nyuma ya kumzuia kwake
lilikuwa ni suala la usalama na ulinzi kwa ujumla”,alisema Mwabulambo.
Chanzo:MADUKA ONLINE
Post a Comment