0

Mara nyingi inakuwa ni shida na tatizo kubwa kufanikiwa kwa wajasirimali wengi wachanga au wanaoanza biashara zao na kuingia katika biashara kwa mara ya kwanza, huku wakiwa wamejaa hofu na uoga mkubwa wa kushindwa katika biashara zao wanazoazisha, hii ni kutokana na wengi wao kuwa na uoga wa kuhofia kuishia njiani na kupoteza mitaji na biashara zao na hatimaye kupata aibu kubwa kwa watu waliowazunguka.

Wapo wajasiriamali wengi walio na hofu ya kufeli katika biashara zao hii ni kwa sababu ya maneno mengi waliyowahi kuyasikia kutoka kwa watu waliokwisha kuwatangulia kwenye biashara hapo mbele, na wakati mwingine yawezekana ni kutokana na watu wa karibu kabisa wanaowaamini kwa mashauri kutoka kwao wamewapa ushauri wa kuwakatisha tamaa badala ya msaada wa kuchukua hatua iliyo salama yenye matokeo chanya zaidi.

Inawezekana umewahi kusikia utafiti kama huu uliowahi kufanyika nchini marekani, utafiti huu unasema kuwa; “kati ya asilimia 90% ya biashara nyingi mpya zinazoazishwa zinafeli baada ya miaka 3 tu.” Kama unakumbana na utafiti kama huu na ni mara yako ya kwanza unataka kuingia katika biashara, uwe na uhakika unaweza kukata tamaa na hata kuacha kutimiza maono yako ya kufanya biashara. Usiogope bali unachotakiwa kufahamu ni nafasi yako unayotakiwa kuitoa ya kujifunza zaidi kila siku ili kujua ni namna gani ya kuepukana na hofu ya kufeli hasa juu ya mambo yote yanayokujengea hofu hiyo ndani yako.

Kuna sababu nyingi sana zinazosababisha biashara nyingi kufeli na kuishia njiani, lakini nataka kukuambia sababu hizo zisiwe ni kisingizio au mchango mkubwa wa kukufanya uogope kuendeleza au kufanya biashara uliyokusudia. Kumbuka njia pekee ya kuepukana na uoga au hofu ya kufeli na kushindwa ni kuamua kulikabili tatizo husika pasipo uoga wowote mbele yako.

Warren Buffett bilionea mwekezaji anayetajwa katika tano bora ya mabilionea na matajiri wakubwa duniani ndani ya mtandao wa forbes aliwahi kusema kuwa, “Warren Buffett said that he would not invest in any business where the owner hasn”t failed at least twice. I love that truly wealthy and successful people understand that failure is part of the process.” Utawekeza vipi katika biashara ambayo haijawahi kupata misukosuko mingi ya kufeli hata mara kadhaa, ni ngumu kujua njia za mafanikio yake. Watu wengi waliofanikiwa wanaelewa na kujua kufeli ni sehemu ya mafanikio ya jambo fulani. Kwa nini wewe unaogopa kufeli? Hakuna mafanikio mazuri nje ya kuanguka au kufeli mara nyingi kama unahitaji kujua na kujifunza zaidi ili kuwa bora.
Hapa kuna mikakati sita ya kukusaidia kuondokana na hofu ya kufeli kama wewe ni mjasiriamali mchanga katika biashara.

1: Elewa kwanza kufeli ni sehemu ya mafanikio yako.
Mojawapo ya sababu kubwa kwa nini watu wengi hasa kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wengi wanafeli katika biashara zao, hii ni kwa sababu hawajajua au kuchukulia kufeli katika biashara au jambo fuani ni sehemu ya mafanikio. Huwezi kukimbia kufeli kama unahitaji kufika katika mafanikio makubwa unayoyataka, kufeli ni sehemu ya maisha ya mwanafunzi anayetaka kujifunza na kujua mambo mengi zaidi ya wengine.

Jambo kubwa unalopaswa kulifamu na kulichukulia hatua katika eneo hili, ni mwenendo mzima kutoka kwako binafsi wa kukubaliana na kufeli kwako au kushindwa ili upate kujifunza zaidi na kutoweza kurudi katika makosa kwa mara ya pili. Kufeli si sehemu ya matokeo hasi tu wakati wote kama wengi wetu tunavyofikiri, bali kufeli kunaweza kuwa ni sehemu mojawapo kubwa ya mafanikio yako. Kumbuka Thomas Edison alifeli mara 1000 katika kutengeneza taa (bulb) ya mwanga wa umeme, lakini alipofuatwa na kuulizwa alikiri hakufeli bali alitumia njia elfu moja alizopata kumfikisha katika mafanikio ya kutengeneza taa hiyo ya mwanga wa umeme.

2: Acha kujilinganisha na watu wengine.
Kila eneo la biashara fulani au kampuni fulani inaweza kujifunza kutoka kwa kampuni nyingine iliyoendelea kuzidi wao binafsi hasa kwa ajili ya kuboresha na kuleta ubora na ufanisi wa kutosha katika eneo la kazi. Hivyo hivyo kwa mjasiriamali au mfanyabiashara binafsi anaweza kutumia mtindo huo ili kuboresha biashara yake na kuleta matokeo chanya na makubwa katika biashara yake aliyonayo.

Unaruhusiwa kujifunza kutoka kwa watu wengine kwa kujipima kwa kutumia eneo la uwezo na udhaifu wako wa kibiashara ulionao kutoka kwako au kwa washindani wako, ila haurusiwi kujilinganisha kwa kutamani kuwa kama wao kwa haraka katika biashara kwani huko ndiko mwanzo wa kuanguka na kufeli kwako moja kwa moja. Wapo watu wanaoingia katika biashara fulani na wakiona fulani kanunua mzigo mpya na yeye anataka kununua mzigo mpya pasipo kuangalia biashara yake au stoo (stock) yake inamruhusu. Hayo ndio makosa yanayoweza kukupelekea kufeli daima.

3: Chukua hatua ya kuendelea mbele kivitendo.
Jambo lingine linaloweza kukusaidia kuondokana na hofu ya kufeli katika biashara kama mjasiriamali mchanga. Kama unatembea katika wasiwasi, mashaka, uoga, hofu na mawazo hasi yanayokusumbua kwa muda mrefu basi huo ndio wakati mazuri na maalum wa kuchukua hatua ya kivitendo kwa ajili ya kuzikabili changamoto hizo zinazokuzuia kusonga mbele kibiashara.

Kwa kukabili hofu na uoga wa kufeli au kushindwa kwa kuchukua hatua za kivitendo, hii inakusaidia kukupa uzoefu na ufanisi wa kufanya kazi zako kwa ubora na uanalifu mkubwa ukifahamu njia zote za kupita ili kufikia mafanikio yako. Wajasiriamali waliofanikiwa wanatumia hofu ya kufeli kama sehemu mojawapo ya kuwahamasisha kuchukua hatua za kivitendo kwa ajili ya kufanikiwa katika biashara zao. Yawezekana ni hofu ya kufeli, hofu ya kuchekwa au kushindwa, hofu ya umasikini, nakadhalika, zote hizi ni vizuri uzitumie kama sehemu ya kukuhamasisha kufanikiwa katika biashara yako na maisha yako binafsi.

4: Acha kuangalia tatizo, bali tafuta majibu ya tatizo husika.
Usijaribu kusahau kuwa biashara yoyote iwe inayotoa huduma au bidhaa; kwa kupitia bidhaa au huduma hiyo inasaidia kuondoa shida na uhitaji mkubwa uliopo katika jamii. Hivyo ni vizuri utumie matatizo yanayojitokeza kama sehemu mojawapo ya fursa za kukusaidia kuongeza ufanisi na ubora wa biashara yako na si kukimbia matatizo husika.

Kama wafanyakazi wako wanalalamikia matatizo yanayojitokeza katika biashara yako, fahamu kuna fursa mpya mahali hapo; kama wateja wako wanapata changamoto na tatizo kubwa la namna ya kupata bidhaa zako, fahamu kuna fursa mpya mahali hapo; kama wasambazaji wa bidhaa zako wanalalamikia ugumu wanaokutana nao katika kusambaza bidhaa zako, fahamu kuna fursa mpya mahali hapo. Nataka kukuambia kwa kadiri changamoto zinavyojitokeza katika biashara yako na kuzichukulia hatua ya kuziondoa ndio kadiri unavyoiweka biashara yako katika ubora na muonekana mzuri wa maboresho.

5: Baki katika mawazo chanya.
Jambo hili ni muhimu pia ulifahamu kama unahitaji kuona matokeo makubwa kwenye biashara yako. Kama wewe ni kiongozi na meneja katika biashara au kampuni fulani unahitaji kufahamu ni muhimu sana kubakia katika mawazo chanya pasipo kutoka hata kama kuna mazingira hasi yanayojitokeza na kutaka kukutoa katika msimamo wako mwema wa kufanikiwa.

Suala la kubakia katika msimamo wenye mawazo chanya ni la msingi sana kama unahitaji kufanikiwa katika biashara yako na kuona mafanikio makubwa nje na ndani ya kampuni ya shirika lako binafsi. Usiogope kupambana na changamoto ndogo zinazojitokeza kwa nje na kutaka kukutoa katika msimamo wa kibiashara. Changamoto kama vile za kukosa wateja kwa muda fulani; kuharibika kwa bidhaa; kunyang’anywa wateja wako; kusemwa vibaya, nakadhalika. Usiogope mambo yote hayo bali baki chanya na kutumia mambo hayo kama fursa ya kukupa hatua nyingine ya juu zaidi.

6: Anza kwa kidogo ulichonacho, ukihesabu mafanikio yako unayoyapata.
Njia mojawapo ya mwisho ya namna ya kuondokana na hofu ya kufeli kwako wewe mjasiriamali mchanga. Jifunze kuanza kwa hicho kidogo ulichonacho na kutumia mafanikio yale madogo unayoyapata kama hatua ya ushindi na sehemu ya kukutia nguvu ili kusonga mbele zaidi. Watu wengi wanaichukulia hatua hii kama sehemu ya kuzuia kupata mambo makubwa kwa haraka, hapana; bali tunafanya hivi ili kukupa msaada wa kukujenga katika kujua wapi unakotoka na wapi unakokwenda ili kujenga ufanisi na ubora mkubwa zaidi katika kazi au biashara.

Mafanikio unayoyapata yanazaa mafaniko mengine. Hivyo hauna haja ya kukimbia mafanikio madogo unayoyapata katika biashara yako kwa kutaka mafanikio makubwa na ya haraka zaidi. Kubali mafanikio madogo unayoyapata ili ufanikiwe zaidi kwa mafanikio makubwa mbele yako.

Namna gani ya kuondokana na hofu ya kufeli katika biashara kama mjasiriamali mchanga unayeanza?
Unaweza ukaacha komenti yako hapo chini kwenye eneo maalum la kukomenti.

Post a Comment

 
Top