Warren Buffett alizaliwa mwaka 1930 katika mji wa Omaha, Nebraska,
Marekani. Baba yake mzazi Howard Buffett, alikuwa akiuza dhamana katika
benki ya Union Street, Omaha 1931. Benki hiyo ambayo baba yake alikuwa
ameajiriwa ilianguka na kufilisika hivyo kujikuta hana ajira na kupoteza
akiba yote. Baba yake aliamua kuanzisha biashara ya udalali wa dhamana,
huku akimsihi mwanae kusoma zaidi.
Warren Buffett alipokuwa shule ya sekondari aliwaeleza wanafunzi
wenzake kuwa atakuwa milionea kabla ya kufikia umri wa miaka 35. Na
alifanikiwa kuwa na dola milioni 6 alipofikia miaka hiyo 35. Warren
alisoma shahada ya uzamili ya uchumi katika Chuo kikuu cha kolombia.
Alijiunga na chuo hiki kwa kuwa alitaka afundishwe na mwalimu bigwa wa
masuala ya uwekezaji, Benjamin Graham. Alipomaliza shahada ya pili,
alijiunga katika biashara ya mwalimu wake Benjamin Graham. Akiwa chini
ya mwalimu wake huyo aliweza kujifunza zaidi masuala ya uwekezaji. Watu
wengine alioweza kujifunza zaidi kutoka kwao ni Charlie Monger, Philip
Fisher, Lawrence N. Boomberg, John B. Williams, Edga Smith, na John M.
Keynes. Katika wote hao aliweza kujifunza masuala mbalimbali
yanayohusiana na uwekezaji katika soko la fedha na masuala ya hisa.
Akiwa kijana mdogo sana, alipita mitaani kuuza kinywaji cha Coke,
akibisha hodi nyumba kwa nyumba na kuweka akiba kwa kila fedha aliyokuwa
akipata na hapo akiwa na umri wa miaka 6. Alinunua chupa moja ya Coke
kwa senti 25 na kuuza kwa senti 50. Akiwa na umri wa miaka 11, alinunua
hisa yake ya kwanza, hisa tatu (3) za kampuni ya Cities Service, kwa
dola 38. Hisa zilishuka bei na kufikia dola 25, lakini hakubabaika
katika hilo. Aliuza hisa zake baadaye na kupata faida ya dola 5. Lakini
baadaye hisa hizi alizouza zilipanda bei na kufikia dola 200.
Alipofikia miaka 19, alianzisha biashara ya kuuza magazeti kwa chini
ya saa mbili kwa kupitia mtandao wa kibiashara aliouanzisha na kujipatia
dola 175 kwa mwezi, aliuza takribani magazeti 500 kila siku. Pia
alijishughulisha na kuuza mipira ya gofu iliyopotea ili kuendelea
kuongeza kipato chake. Aliwahi kumiliki gari ya Roll Royce kwa ubia na
kujipatia dola 35 kwa siku.
Warren Buffett aliamua kuanzisha kampuni yake ya Berkshire Hathaway
baada ya kugundua kuwa haitoshi kujifunza biashara kwa kusoma kitabuni
au kuhudhuria kozi tu bali kwa vitendo zaidi. Hadi hapo alikuwa
amefanikiwa kusoma kitabu maarufu cha uwekezaji (The Intelligent
Investor), kitabu anachokiri hadi kesho kuwa kilimfungua maisha yake
kuhusu uwekezaji mwaka 1950, hapo akiwa bado na miaka 19.
“Price is what you pay. Value is what you get.” -Warren Buffett
Alipotoka shuleni, alipenda sana kusoma magazeti yenye habari ya soko la hisa la Marekani (Wall street journals)
na taarifa za mwaka za makampuni mbalimbali. Alisoma zaidi ya vitabu
100 vya uwekezaji kwa kipindi kifupi. Hata walimu wake shuleni,
walipenda sana kumuuliza na kumwomba ushauri kuhusu uwekezaji. Pamoja na
kupenda kusoma taarifa kuhusu masoko ya hisa na dondoo motomoto,
majedwali na michoro hayakwenda vizuri sana. Hakuwa na mbinu na mikakati
madhubuti ya uwekezaji mpaka alipompata mwalimu wake Benjamin Graham wa
Chuo Kikuu cha Kolombia, mwaka 1950. Warren Buffett alikuwa na bidii
shuleni na kupata alama za juu A+ wakati akisoma shahada ya pili ya
uzamili ya uchumi.
Mwaka 1958 alinunua nyumba yake ya kwanza kwa dola 31,500 na bado
anaishi katika nyumba hiyo hadi hivi leo. Ni mmiliki wa kampuni ya
Berkshire Hathaway. Ni kati ya wakurugenzi watendaji wanaolipwa mshahara
mdogo kwa mwaka dola 100,000 ukilinganisha na wakurugenzi wengine
katika makampuni mengine makubwa duniani. Hupenda kula katika hoteli za
kawaida kuliko kwenda hoteli za kifahari, na kinywaji chake akipendacho
cha Coke. Warren siyo mfuja fedha na hana matumizi mabaya ya fedha na
mojawapo ya tabia yake ni kuwa “fedha ni lazima ihifadhiwe na kutunzwa vizuri (preservation of capital).’ Aliwahi kutoa takribani dola bilioni 30 kwa Bill na Melinda Gates Foundation kusaidia miradi ya maendeleo.
Hadi hivi sasa Warren Buffett ni tajiri wa tatu duniani akiwa ana
utajiri unaofikia $60.8 Bilioni kwa mujibu wa jarida la Forbes la nchini
Marekani. Nakumbuka siku moja nilisoma kijana mmoja aliwahi kumuomba
ushauri afanye kitu gani ili aweze kufanikiwa, Warren Buffett alimwambia
asome kurasa (pages 500) kwa siku. Hii ni wazi kuwa Warren anatuonesha
umuhimu wa kusoma vitabu kama sehemu mojawapo ya kupata ufahamu na
taarifa nyingi za kuweza kukusaidia kufanikiwa. Kama Warren anasoma
kurasa 500 kwa siku pamoja ana kazi kubwa ya kuendesha kampuni
aliyonayo, Jiulize mimi na wewe tunasoma kurasa ngapi kwa siku?
Mambo 5 Ya Kujifunza Kutoka Kwa Warren Buffett:
1: Umri wako mdogo si kigezo cha kuacha kuifata ndoto yako na kuitimiza.
Wapo watu wengi huwa wanaona kama kuna muda fulani maalum kwa ajili
ya kutimiza ndoto zao walizonazo, wengine wanaamini umri wa kufanikiwa
ni kuanzia miaka 45 au 50 nakuendelea. Wapo wanaoamini kuwa milionea au
bilionea kwenye umri mdogo ni kitu kigumu sana, hapana. Warren Buffett
akiwa na miaka 35 alikuwa tayari amefanikiwa kutimiza ndoto yake
aliyokuwa nayo ya kuwa milionea. Unachopaswa kuelewa ni kufahamu unataka
nini kwenye maisha yako, simamia kitu unachokipenda na shikilia
ulichonacho hadi uone matokeo yakitokea juu yake. Usikubali umri uwe
kikwazo cha kutimiza maono na ndoto yako kubwa uliyonayo katika maisha
yako.
Kijana wa kimarekani Evan Spiegel ambaye ni mwanzilishi na mmiliki wa
Snapchat ni miongoni mwa vijana wadogo duniani akiwa na umri wa miaka
25 hadi sasa, lakini ni miongoni mwa mabilionea duniani, mwenye utajiri
unaofikia dola 2.1 bilioni (zaidi ya trilioni 5.2) na kumfanya kuwa
kijana mdogo mwenye pesa nyingi zaidi. Mara baada ya kusoma katika shule
ya crossroads, akamalizia elimu yake katika Chuo cha Stanford kilicho
nchini Marekani. Baada ya kuona mitandao ya kijamii ikishika kasi,
akamua kuungana na mwenzake Bobby Murphy kwa ajili ya kutengeneza
mtandao wao wa kijamii wa Snapchat ambao umekuwa maarufu duniani kwa
sasa. Umri wako si kigezo cha kushindwa kufuata na kutimiza ndoto zako,
amini unaweza na amka leo kuifata ndoto yako pasipo kusubiri kesho.
2: Tafuta maarifa na taarifa sahihi juu ya eneo unalotaka kufanikiwa.
Mara nyingi watu wengi wamejaribu kuingia kufanya biashara au
uwekezaji fulani pasipo kupata taarifa sahihi zenye kuweza kuwasaidia
katika kufanikiwa vyema katika maeneo hayo. Hii ndio sababu ya watu
wengi kuishia njiani na kushindwa kufanikiwa katika vitu vingi
wanavyoanzisha na kuanza kufanya. Warren Buffett alijifunza uwekezaji wa
Hisa baada ya kujenga tabia ya kusoma vitabu zaidi na mojawapo ya
vitabu alivyovisoma na kumpa maarifa aliyokuwa akitaka, The Intelligent Investor, Security Analysis, na Common Stock and Uncommon profits.
Jiulize ni mara ngapi umetoa muda wa kujifunza au kutafuta ujuzi fulani
kwa ajili ya kufanikisha malengo na ndoto yako kubwa uliyonayo?
Kwa mara ya kwanza nilishangaa sana kusikia Warren Buffett anasoma
kurasa 500 kwa siku. Hii ni wazi tajiri huyu anafahamu umuhimu wa
maarifa katika kumsaidia kufanikisha malengo yake aliyonayo. Watu wengi
wanaotaka kufanikiwa leo hii si wepesi wa kujitoa katika kutafuta
maarifa na taarifa sahihi kwa gharama yoyote ili kujijenga kiufahamu
katika vitu wanavyotaka kuvifanya. Jiulize mara ya mwisho kusoma kitabu
ilikuwa ni lini? Huwezi kuvuka eneo moja kwenda eneo jingine kwa kupitia
ufahamu au maarifa yale yale uliyokuwa nayo tangu mwaka jana.
“Some people dream of success, while others wake up and work hard at it.” -Mark Zuckerberg
3: Kuwa karibu na watu wenye uwezo kwa ajili ya kukuongoza na kukushauri.
Kuwa karibu na watu wenye uwezo na uzoefu kuliko wewe kunaweza
kukusaidia katika kukupa mbinu nyingi zaidi za kukuwezesha kuvuka
vikwazo na changamoto kwa wepesi ili kufanikisha ndoto yako. Usijaribu
kutafuta mchawi wa mafanikio yako kwa kujaribu kufanya kila kitu peke
yako, ili uvuke changamoto zinazoonekana ni ngumu kwako ni vizuri zaidi
utafute watu walio na uwezo na uzoefu kuliko wewe ili wakushauri mara
kwa mara katika kitu unachotaka kukifanya. Jifunze kuwa na mshauri
(mentor) kwenye kila eneo unalotaka kufanikiwa katika maisha yako.
4: Ili ufanikiwe kifedha unahitaji kuwa mwangalifu katika matumizi yako ya fedha ya kila siku.
Warren Buffett hakutokea familia yenye uwezo sana ila baba yake
alikuwa mfanyakazi wa benki kabla benki hiyo haijafilisika na kutafuta
kazi nyingine ya kufanya ili kujipatia kipato. Akiwa na miaka 6 Warren
ndio alipoanza kuzunguka mitaani na kuuza kinywaji cha Coke, na kila
fedha aliyoipata alijifunza kuihifadhi kwa kuweka akiba hadi pale
alipotimiza miaka 11 akaanza kununua hisa. Hii inatuonesha wazi kuwa
Warren Buffett alikuwa ni kijana smart na mwangalifu sana katika
matumizi yake ya fedha na hiki ndio kitu kilichomsaidia kufikia kuwa
milionea akiwa na miaka 35 kama alivyowatamkia wenzake akiwa shuleni.
Leo hii jiulize ni mara ngapi unapopata fedha baada ya
kujishughulisha na kitu fulani unachofanya huwa unaheshimu na kutumia
fedha zako kwa matumizi muhimu ili kutoa nafasi ya kuweka akiba na
kuongeza thamani ya fedha yako kuongezeka. Usipojifunza namna nzuri ya
matumizi ya fedha zako utabaki kuota ndoto za utajiri pasipo kuona
uhalisi wowote katika maisha yako. Hakuna utajiri anaoweza kuupata mtu
nje ya nidhamu anayoweza kuijenga katika matumizi yake ya fedha. Jifunze
kuweka akiba na kujua njia nzuri za kuwekeza fedha zako mahali sahihi
palipo na faida ili kukutengenezea utajiri mkubwa.
5: Jifunze kutoa kuliko kupokea.
Warren Buffett inakadiriwa ndio tajiri aliyewahi kuweka historia ya
kurudisha fedha nyingi zaidi kwa jamii baada ya kutoa takribani dola
bilioni 30 kwa Bill na Melinda Gates Foundation kusaidia miradi ya
maendeleo. Hii ni wazi kuwa tajiri huyu anafahamu siri kubwa ya
kufanikiwa zaidi ni kurudisha kwa jamii kile alichonacho. Kumbuka ili
ufanikiwe zaidi unahitaji kujifunza namna ya kutoa kuliko kupokea tu.
Kutoa ni pamoja na kidogo ulichonacho sasa, usisubiri ufanikiwe kama
Warrren Buffett ndio uanze kujifunza kutoa. Anza kujenga tabia ya kutoa
kuanzia sasa ili utakapofanikiwa kesho watu wengi wazidi kufaidi matunda
ya kufanikiwa kwako.
Post a Comment