Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako
***
SERIKALI imezitaka shule zote za msingi na sekondari binafsi
zilizowafukuza ama kuwataka wazazi na walezi kuhamishia watoto wao shule
zingine kwa kigezo cha kutofikia wastani wa ufaulu, kuwarudisha mara
moja shuleni bila masharti yoyote.
Agizo hilo limetolewa na Kaimu Kamishna wa Elimu wa Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia, Nicolas Buretta kupitia taarifa yake kwa vyombo
vya habari ambayo imeeleza kuwa wizara hiyo imebaini kuwepo kwa shule
zisizo za serikali na hasa zinazomilikiwa na mashirika ya dini
zilizokiuka utaratibu wa elimu nchini kwa kufanya matendo hayo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa shule hizo pia zimeendelea kukaririsha,
kuhamisha shule nyingine darasa au kuwafukuza wanafunzi hao katika shule
kwa kigezo hicho.
Wizara hiyo imezitaka shule zote zilizowataka wazazi na walezi
kuwahamishia watoto wao katika shule nyingine kwa kigezo cha kutofikia
wastani wa ufaulu wa shule kufuta agizo hilo na kuendelea na wanafunzi
hao bila masharti yoyote.
“Wazazi na walezi wenye wanafunzi waliorudishwa nyumbani kwa sababu
hizo, wahakikishe wanawarudisha watoto wao kwenye shule walizokuwa
wakisoma ili waendelee na masomo kama kawaida,” ilieleza sehemu ya
taarifa hiyo.
Aidha, imezitaka shule hizo kuwa na utaratibu wa kuinua viwango vya
taaluma kwa wanafunzi wenye ufaulu mdogo badala ya kukaririsha darasa
kwa kigezo cha kutofikia wastani wa ufaulu uliowekwa na shule, na kwamba
ikitokea ulazima wa kufanya hivyo taratibu zilizopo zifuatwe.
Katika hatua nyingine, Buretta amewataka wadhibiti wa ubora wa shule,
kanda na wilaya kusimamia utekelezaji wa agizo katika maeneo yao yote,
huku akionya kuwa shule yoyote itakayokiuka agizo hilo itachukuliwa
hatua kwa mujibu wa sheria.
Agizo hilo liliwahi kutolewa na Waziri wa Elimu wakati huo, Dk Shukuru
Kawambwa ambaye alipiga marufuku shule hizo kuwasitishia masomo
wanafunzi wanaoshindwa kufikisha wastani wa ufaulu wa shule huku akiweka
wazi kuwa atakayekaidi agizo hilo atafutiwa usajili.
Kitendo hicho kimeelezwa kuwa ni kinyume na miongozo iliyotolewa na
Wizara hiyo na kimesababisha baadhi ya wanafunzi kushindwa kuendelea na
masomo na hivyo kupoteza haki yao ya msingi.
Waraka wa Elimu namba 12 wa mwaka 2011 umeeleza kuwa ni marufuku kwa
shule kukaririsha, kuhamisha au kufukuza wanafunzi kwa kushindwa
kutimiza wastani wa alama za ufaulu uliowekwa na shule.
Mwanafunzi yeyote aliyedahiliwa kujiunga na masomo anapaswa kuendelea na
masomo isipokuwa kama atashindwa kufaulu mtihani wa taifa uliowekwa na
wizara pekee.
Chanzo-Habarileo
Post a Comment