0



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amelazimika kuendesha harambee ya papo kwa papo na kuchangisha sh.milioni 138.26 ili kufanikisha ujenzi wa shule mpya ya sekondari wilayani Ruangwa.
Hatua hiyo hiyo inafuatia wingi wa wanafunzi waliofaulu mtihani wa darasa la saba na kuchaguliwa kuingia kidato cha kwanza lakini hawakufanikiwa kupata nafasi katika mkupuo wa kwanza.

Katika harambee iliyofanyika kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Ruangwa leo mchana Waziri Mkuu amefanikisha kupatikana kwa fedha kiasi cha sh. milioni 120.65 na mifuko 550 ya saruji  na mabati 360 (vyenye thamani ya sh. milioni 17.61) ambavyo vitatumika kujenga madarasa manne ya kidato cha kwanza yanayotakiwa kuwa yamekamilika ifikapo Januari 15, 2017.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Andrea Chezue, jumla ya watoto 319 walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza lakini walikosa nafasi sababu ya ukosefu wa madarasa na walitakiwa kusubiri hadi chaguo la pili ambalo kwa kawaida hufanyika Februari, kila mwaka.
        Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo hilo, amechangia sh. milioni 33 kutoka kwenye mfuko wa jimbo ili kuharakisha ujenzi wa madarasa mawili ya kuanzia.
Waziri Mkuu amewashukuru wote waliojitolea kuchangia ujenzi wa shule hiyo. Amerejea jijini Dar es Salaam jioni hii.

Post a Comment

 
Top