0

Mkuu  wa  mkoa  wa LIndi  Godfrey  Zambi  akizungumza kwenye  mahafali ya tatu  ya  VETA LINDI

Waandishi  wetu
WADAU mbalimbali wa maendeleo mkoani Lindi,wameombwa kuwahamasisha vijana wakiwemo wa kike kujiunga na vyuo vya ufundi, kikiwemo cha Veta,ili wapate utaalamu utakaowasaidia kuendesha maisha yao ya sasa na baadae.
 
Ushauri huo umetolewa na mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi na huduma mkoani humo,Samwel Ng’andu alipokuwa anatoa taarifa ya utekelezaji, kwenye mahafari ya tatu ya wahitimu 108,yaliyofanyika viwanja vya Chuo hicho kilichopo mjini Lindi.
 
Akiwasilisha taarifa hiyo,ambapo mgeni rasmi alikuwa mkuu wa mkoa huo,Godfrey Zambi,Ng’andu alisema tangu Chuo hicho kianzishwe kutoa mafunzo miaka minne iliyopita,idadi ya waschana kujiunga na Chuo sio ya kuridhisha,ikilinganishwa na mikoa mingine hapa nchini.
 
Ng’andu alisema tangu kuanzishwa kwa Chuo hicho cha Veta mwaka 2012,kimeweza kudahili wanafunzi 1,122 kati yao wavulana 834 na waschana 279 sawa na asilimia 24.5%.
 
Alisema kila mwaka Chuo hicho kinadahili wanafunzi ambapo kwa mwaka huu 2016,waliodahiliwa ni 280 kati yao waschana (29) tu,na kufanya waschana wote waliokwisha dahiliwa tangu kuanzishwa kwa Chuo hicho,miaka miaka mitano iliyopita kufikia waschana 65,idadi ambayo sio ya kuridhisha ndani ya mkoa huo.
 
Mkuu huyo wa Chuo cha Veta Lindi alisema ndani ya kipindi cha miaka minne, kuanzia mwaka 2013 hadi 2016,kimeshatoa mafunzo kwa washiriki wapatao 1,497 wakiwemo wanaume 1,366 na wanawake 131 sawa na asilimia 9%,idadi ambayo ni ndogo ikilinganishwa na uwezo wa Chuo.
 
“Mh,mgeni rasmi Chuo chetu cha Veta hapa Lindi,kina uwezo mkubwa, lakini tatizo lililopo ni idadi ndogo ya watu kujitokeza kujiunga nacho”Alisema Ng’andu.
 
Akizungumza wakati wa mahafari hayo ya tatu,mkuu wa mkoa wa huo, Godfrey Zambi,amewataka wananchi kuchangamkia fursa hiyo,kupata mafunzo ya ufundi Stadi kupitia Chuo cha Veta cha Lindi,huku akipongeza jitihada zinazofanywa na viongozi kuweza kupanua wigo wa mafunzo.
 
Zambi pia amewataka wahitimu hao 108,kuwa mabalozi wazuri wanaporejea uraiani,ikiwemo kuyatumia mafunzo waliyoyapata kwa kujiajili wao wenyewe,ili kujiletea maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
 
Chuo cha ufundi Stadi na huduma (Veta) mkoani Lindi,kilizinduliwa Apri 10/2012 na aliyekuwa makamu wa Rais wa Tanzania awamu ya nne,Dakta Mohamedi Gharib Bilali,kinaendesha fani mbalimbali, zikiwemo useremala,umeme,uunganishaji vyuma,uhaziri,ushonaji na utengenezaji wa magari.

Post a Comment

 
Top