0

Mojawapo ya kikwazo kingine kikubwa cha mafanikio katika maisha ya mtu, ni tabia ya kusikiliza wanachoongea watu wengine juu yake hata kama hakina ukweli wa maana ndani yake. Kama unataka kufanikiwa ni vizuri ukajifunza kuheshimu kwanza mawazo yako uliyonayo yanayokupa msimamo juu ya ndoto yako kabla ya mawazo ya nje. Usikubali mawazo ya wengine kuwa namba moja kukukwamisha katika safari yako ya mafanikio. Hii ndio maana unapaswa kuwa makini katika kuchagua ni watu gani wa kuwa nao katika maisha yako, tafuta watu chanya wenye kuweza kukupa hatua dhidi ya maono yako uliyonayo.
Jifunze kusikiliza sauti yako ya ndani inayokusemesha kwa ajili ya hatima yako na mafanikio unayotaka. Kumbuka karibu asilimia 90 ya mafanikio yako yanahitaji msimamo wa kudumu unaoanzia ndani yako. Amua kujifunza mara kwa mara mambo yanayoweza kuifanya sauti yako ya ndani kuwa halisi kila wakati juu ya mafanikio unayotaka ili uweze kujenga misingi chanya ya kukupeleka katika kilele cha ndoto yako. Ukweli ni kuwa kadiri unavyolisha akili na moyo wako mambo chanya zaidi ndivyo sauti yako ya ndani inakua halisi na kukuelekeza mahali sahihi unapota kufika.
Tumia kelele za wengine kama nganzi ya kukupandisha kwenye kilele chako cha mafanikio. Ila usikubali kuumia au kutokusonga mbele kwa sababu ya mawazo au maneno mabaya wanayokuwazia watu wako wa karibu. Jifunze kuamini mafanikio juu yako hata kama hakuna mtu anayeamini unachokiamini kwa Sasa. Utakapoanza kuamini wewe binafsi juu kile unachokitaka na kuchukua hatua bila kuchoka, hii itakufanya uweke uhalisi utakaowafanya walio kuzunguka kuona matokeo ya kile ulichokuwa ukitafuta kwa muda mfupi. Jifunze kunyamaza, ongeza hatua.
Husiwe mmojawapo wa watu wanaoishi kwa kuangalia maneno ya watu. Amua kupiga hatua ISHINDOTOYAKO usitazame nyuma, songa mbele. Ziba masikio yote mawili zidi ya kelele zote zinazokuzuia kuifata ndoto yako. Narudia kukuambia ziba masikio yote mawili na amua kuishi ndoto yako.

Post a Comment

 
Top