Kumekuwa na taarifa inasambazwa katika
mitandao ya kijamii, makundi ya ‘WhatsApp’, ‘Facebook’ na majukwaa
mbalimbali ikieleza kuwa Serikali imepiga marufuku watumishi wa umma
kukopa Benki,SACCOS,VICOBA na Taasisi mbalimbali za kifedha.
Taarifa iliyotolewa leo tarehe 20 Desemba 2016 na Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali imeeleza kuwa taarifa inayosambazwa, ambayo imetafsiri
mawasiliano ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni ya kupotosha,
hivyo watumishi wote wa umma wanaombwa kuipuuza.
Vilevile watumishi wa umma wametakiwa kuzingatia kuwa Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali HAINA mamlaka ya kuzuia wala kuruhusu
mtumishi yeyote wa Serikali kukopa au kutokopa katika Taasisi yoyote ya
Fedha nchini.
Watumishi wa umma pia wamekumbushwa kuwa mikopo yote ya watumishi wa
umma katika Taasisi za Fedha hutolewa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na
taratibu zilizopo ili mradi mtumishi awe ametimiza vigezo.
Aidha, watumishi wa umma wameaswa kuacha tabia ya kusambaza taarifa
zisizo za kweli na ambazo zina mamlaka husika ya kuzitoa ikiwa ni pamoja
na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.

Post a Comment