0


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein amezipongeza juhudi zinazochukuliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika AFDB kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo.



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) Dk.Tonia Kandiero alipofika Ikulu Mjini Unguja leo.


    Akizungumza na aliyekuwa mwakilishi wa AFDB zanzibar, Dkt. Tonia Kandiero ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kuagana baada kupewa majukumu mengine ya kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya AfDB Kusini mwa Afrika, Dkt. Shein amesema Benki hiyo imekuwa ikichukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha miradi mbali mbali ya maendeleo hapa Zanzibar inaimarika na kuendelea kuwasaidia wananchi wote. 




Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akiagana na  Mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) Dk.Tonia Kandiero alipofika Ikulu Mjini Unguja leo baada ya mazungumzo yao,[Picha na Ikulu. 21/12/2016 



Dkt. Shein amesema kuwa mbali ya Benki hiyo kutoa ushirikiano wake katika kuimarisha sekta za maendeleo hapa nchini  zikiwemo maji, barabara, kilimo, nishati, afya, elimu na utawala bora pia, imeweza kutoa mashirikiano katika nyanja nyengine za kijamii, kiuchumi na kimaendeleo.
  Kwa upande wake Dkt. Kandiero amemuhakikishia Rais Shein kuwa miradi yote inayosimamiwa na Benki hiyo itakamilishwa ikiwemo miradi ya ujenzi wa barabara zikiwemo barabara ya  Mahonda -Mkokotoni yenye urefu wa km 31, Fuoni -Kombeni km 8.6, Pale- Kiongele km 4.6 na Matemwe - Muyuni yenye urefu wa km 7.6.

Pamoja na hayo, Dk. Kandiero ambaye amefanya kazi zake hapa Tanzania kwa takriban miaka sita, amemueleza Dkt. Shein kuwa AFDB itaimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na kutoa  pongezi za pekee kwa Dkt. Shein na serikali anayoiongoza kwa kusimamia vyema miradi ya maendeleo.







Post a Comment

 
Top