Wakazi
wa Kijiji cha Tambani Kata ya Tambani wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani,
wamemwomba Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa kukihamishia kijiji hicho Mkoani Dar es Salaam kutoka Mkoa wa
Pwani, kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya miundombinu na
upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii.
Wakizungumza
katika mkutano wa kupitisha azimio hilo kijijini hapo, Wakazi hao ambao
kwa mujibu wa mwenyekiti wao Amiri Abdallah Mbamba idadi yao inafikia
6,013 kwa kipindi chote wanaishi bila kuwa na mawasiliano na wilaya ya
Mkuranga, badala yake huduma zote wanazipata kutoka wilaya za Ilala na
Temeke zote za Mkoa wa Dar es Salaam.
Maelezo
ya wananchi hao ni kwamba wanapohitaji huduma za kiutawala
zinazopatikana wilayani Mkuranga, wanalazimika kupitia Mbagala mkoani
Dar es Salaam kabla ya kufika Makao makuu ya wilaya hiyo umbali wa
kilomita 30, wakati huduma hizo wangezipata katika wilaya za Ilala ama
Temeke ambako ni karibu zaidi na kwa gharama nafuu, wakitolea mfano
nauli ya kwenda Mkuranga ni shilingi 4,000 wakati kwenda Ilala ni
shilingi 600 tu.
Katika
mkutano huo, ilielezwa pia kwamba kutokana na jiogrofia ya kijiji,
halmashauri ya wilaya ya Mkuranga kwa kipindi kirefu imeshindwa
kutengeneza miundombinu ya barabara na daraja linalounganisha kijiji
hicho na vijiji vingine, wakati huduma za doria za ulinzi na usalama
hazipatikani hadi msaada kutoka mkoa wa Dar es Salaam.