0

Moja ya imani ambayo imekuwa ikileta malumbano katika jamii ni kuhusu mtoto kubemendwa, ikimaanisha mtoto aliyezaliwa kutopiga hatua za ukuaji au kulemaa viungo vya mwili.

Dhana hii iliyoonea maeneo ya Pwani hususan mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Tanga na Morogoro inaelezwa kuwa inatokana na wazazi wa mtoto kujihusisha na mapenzi pindi anapokuwa bado mchanga.

Wengine huwaita watoto hao kwa majina ya kukejeli ikiwamo ‘fundi viatu’, kutokana na mwonekano wa mtoto ulivyo, kwani huwa hawezi kutembea, kutambaa wala kuongea.

Wapo wanaosema kuwa chanzo cha watoto kupata hali hiyo, ni pale wazazi wanaposhiriki tendo la ndoa kupita kiasi wakati mtoto akiwa bado mchanga na ananyonya.

Sababu nyingine ni mwanamke mwenye mtoto mdogo kujihusisha na uzinzi nje ya uhusiano akiwa bado ananyonyesha mtoto.

Inaelezwa kuwa mwanamke anapofanya ngono huku mtoto akiwa ananyonya, mtoto anaweza kunyonya maziwa yaliyochanganyika na mbegu za kiume na hivyo kumdhuru.

Wazazi wanaokumbwa na kadhia hii huwaficha watoto wao au hata kuhama makazi kwa kuhofia aibu. Kibaya zaidi ni pale wazazi wanapotuhumiana na kisha kufarakana kwa sababu ya hali hiyo.

Upi ukweli?
Kwa namna tukio la kubebemendwa kwa watoto linavyoelezwa na wanajamii, ni dhahiri linahusiana moja kwa moja na tatizo la mtoto aliyezaliwa na kushindwa kupiga hatua za maendeleo ya ukuaji wa kimwili, kiakili na kijamii.

Pia, inahusu watoto waliopata jeraha la kudumu la ubongo na hivyo kupooza viungo au kuwa na viungo vyenye kulemaa na kuchelewa kupiga hatua za ukuaji; kitaalamu tatizo hili hujulikana kama ‘Cerebral Pulse’.

Kitabibu, mtoto mwenye ukuaji hafifu huwa na kawaida ya kuwa mfupi na uzito huwa ni mdogo, kulinganisha na watoto wengine wenye umri sawa.

Kwa wale waliofikia ujana wanaweza kuonekana wakiwa wamedumaa na huku wakiwa na mabadiliko yasiyo ya kawaida wakati wa balehe.

Kimsingi, kubemenda mtoto ni dhana na imani potofu. Kisayansi na kitiba kufanya mapenzi hakusababishi mtoto kuduma au kutokuwa na uwezo wa kukua.

Pia, sio sahihi kuwa mbegu za kiume zinaweza kupenya na kuingia katika mfumo wa damu wa mama na kufika katika vifuko vya maziwa na kisha kumwathiri mtoto anayenyonya.

Kwa kawaida mbegu hizo hubebwa na majimaji mazito na hatimaye kuingia katika nyumba ya uzazi na kubaki huko. Zinazobaki hushuka na kutoka ukeni mwanamke anapokuwa amesimama na nyingine huvunjwahuvunjwa au kuharibiwa na vimeng’enya vya mwili na kutoka pamoja na uchafu mwingine.

Inawezekana kama baadhi ya watu wanavyosema, wazee wa zamani walitunga uongo huu, ili kuwatisha watu wasishiriki tendo la ndoa baada ya mwanamke kujifungua.

Ni kweli siyo vyema kushiriki tendo la ndoa mara baada ya kujifungua. Kitaalamu tunashauri angalau zipite wiki sita au siku 40, kama ilivyozoeleka kijamii; hii inaepusha kupata maambukizi ikiwamo ya nyumba ya uzazi.

Kwa kawaida wiki za mwanzo baada ya kujifungua mazingira ya uke yanakuwa na unyevu pamoja na mabaki au majimaji yaliyochanganyika na damu ambayo yanaweza kuwa ni mazalia ya vimelea. Mabaki hayo yanaweza kuacha kutoka baada ya wiki mbili mpaka nne.

Sababu za kitabibu zinazochangia mtoto kutokukua
Watoto wenye tatizo la ukuaji, huonekana wakiwa na ukuaji hafifu kwa upande wa tabia za kimaumbile, ikiwamo kushindwa kutambaa, kukaa, kusimama na kutembea. Pia, huwa na maendeleo ya taratibu kiakili, kijamii na tabia zinazoashiria jinsia yake ikiwamo kubalehe.Kwa kawaida mtoto hupitia hatua mbalimbali za ukuaji na kila hatua huwa na tabia zake. Kwa mfano, mtoto anapokuwa mchanga ndani ya miezi miwili anatakiwa awe amekaza shingo au anapokuwa na mwezi mmoja awe anatabasamu kwa watu wa karibu.

Yapo matatizo mengi ya kitabibu yanayoweza kusababisha mtoto asiweze kupiga hatua za ukuaji kama kawaida.

Tatizo hili linaweza kuonekana zaidi katika jamii zenye hali duni za kiuchumi, ikiwamo maeneo yenye ukame, vita vya wenyewe kwa wenyewe na wakimbizi.

Mtoto kama hapati maziwa ya mama na lishe (kwa waliofikia miezi sita na kuendelea) kama invyopendekezwa, anaweza kukumbwa na tatizo hili.

Kwa mfano, mtoto mdogo wa chini ya miezi sita anatakiwa kunywa maziwa ya mama pekee; anyonyeshwe angalau mara nane mpaka 10 kwa siku.

Inawezekana mama akawa hana ujuzi wa kumnyonyesha katika mtindo sahihi, hivyo kuchangia mtoto kutopata maziwa ya kutosha. Aidha, ni makosa kuwaanzishia watoto vyakula vya kulikiza (vya kawaida) kabla ya kufikia umri wa miezi sita.

Sababu nyingine ni mtoto kulishwa chakula katika mazingira yasiyofaa kama vile kulishwa akiwa anatazama runinga, kuwa eneo lenye fujo au kutolishwa kwa ratiba.

Matatizo mengine ni pamoja na hitilafu katika chembe za urithi hali inayochangia kupata mtindio wa ubongo, kitabibu hujulikana kama Down syndrome na kuzaliwa na hitilafu katika ogani kubwa ikiwamo moyo na figo.

Pia, matatizo ya tezi zinazozalisha kichochezi cha ukuaji wa mwili, madhara katika ubongo au mfumo wa fahamu ambayo yanaweza kusababisha mtoto kushindwa kula, maradhi ya moyo na mapafu yanayoweza kusababisha utawanyaji hafifu wa oksijeni na virutubisho mwilini.

Upungufu wa damu na matatizo katika chembe za damu, matatizo sugu ya kiafya mfumo wa chakula, kupata jeraha la ubongo wakati kuzaliwa (cerebral palsy) na ujauzito kupata madhara na kujifungua njiti au uzito mdogo sana.

Sababu nyingine ni pamoja na kuumizwa kihisia kutokana na kuondokewa na wazazi, kutengwa au majanga ya kijamii.

Wito kwa jamii
Kitaalamu hakuna dhana ya kubemenda mtoto hasa tukio hilo linapohusianishwa na kitendo cha kujamiiana. Tatizo la ukuaji kwa watoto linatokana na sababu za kiafya na kimazingira.

Wazazi wazingatie elimu ya afya inayotolewa katika vituo vya huduma za afya vinavyotambulika. Kina mama wahakikishe wanafika katika kiliniki za wajawazito na kupata huduma na ushauri.

Post a Comment

 
Top