Nini unachoweza kufikiri kwa mara ya kwanza pale unapoambiwa kukubali
kudharaulika kunaweza kukuongezea nguvu ya kufanikiwa kule unapoelekea,
tofauti kabisa na ulivyowahi kufikiri hapo kabla? Ni rahisi kunifikiria
vibaya na kusema nimechanganyikiwa. Yawezekana kwa namna yoyote
utakavyofikiri, lakini Je, hizi ni fikra sahihi kwangu? Ukweli ni kwamba
kama unajihisi unapitia mahali pa kudharaulika kwenye eneo fulani
katika maisha yako, basi una nafasi kubwa ya kuweza kufanikiwa kama
utasimama imara katika nafasi yako sahihi pasipo kuteteleka.
Wakati watu wengine wanatumia muda mrefu kukudhoofisha na kukufanya
uonekane mnyonge katika maisha yako, hasa kwa sababu ya kuangalia hali
yako na mahali ulipotoka kifamilia, kiwango chako cha elimu pamoja na
kiwango chako cha kiuchumi; haupaswi kuzingatia kila jambo wanalokusema
na kukunyoshea kidole bali amini katika uwezo mkubwa ulionao ndani yako.
Fahamu kudharaulika kwako kunakuandaa katika nafasi ya juu (greatness)
ya mafanikio yako.
Hapa chini nimekupatia sababu 3 kwa nini kujishusha na kuonekana mdogo kunaweza kukupa nafasi ya kuwa mshindi:
1: Historia inathibitisha jambo hili. Watu waliodharaulika ndio waliotawala.
Kutokea kipindi cha Daudi na Goliathi hadi Donald Trump, historia
inatuonyesha kwamba kukubali kudharaulika na kuonekana hufai kwa kipindi
fulani, hiyo ndio imekuwa ni silaha na siri kubwa ya mafanikio na
ushindi wa watu wengi duniani. Katika historia ya kweli inayomuhusu
Daudi na Goliathi, utaona Daudi pamoja na udogo wake aliokuwa nao hata
kufikia kudharaulika na jitu kubwa lenye uwezo alilokuwa akipambana
nalo; hii haikumfanya Daudi kuangalia majigambo na dharau za Goliathi na
watu wake wa karibu bali aliamua kupambana hadi alipopata ushindi.
Kejeli za maadui zake hazikumpunguzia ari yake (moral) ya kutafuta
kushinda sawa na picha ya halisi aliokuwa amebeba ndani yake.
Ilikuwa si rahisi sana kwa watu wa upande wa Goliathi na hata baadhi
ya ndugu zake na Daudi, kuamini kuwa Daudi anaweza kushinda vita ile na
kufikia kumwua na kumwangamiza Goliathi kwa haraka. Na hiki ndio
tunachokiona kwa mshindi wa uraisi katika taifa la Marekani Donald
Trump. Pamoja na kusemwa sana na hata kudharaulika na watu wengi kwamba
hatofanikiwa kushinda na kushika nafasi ya uraisi, Donald Trump
ameithibitishia dunia yote baada ya kuwa imara na hata kuwa mshindi wa
kinyanganyiro hicho cha uraisi katika taifa kubwa duniani. Unahitaji
kutokukata tamaa hata kama watu wote hawataamini uwezo mkubwa ulionao
ndani yako, amua kuamini ndoto yako hadi utakapoona ushindi ukitokea
mbele yako. Jifunze kwa Daudi na Trump na watu wengine waliofanikiwa
kisha amua kuchukua hatua juu ya ndoto yako.
“When I write, I try to represent the voices of people I’ve known who had no voice.”
―Carla H. Krueger
2: Unapoonekana hufai ndio wanakuongezea umakini (focus) na kujifunza zaidi.
Siku moja wakati naangalia filamu ya Jaden Smith ambaye ni mtoto wa
mwigizaji maarufu wa Marekani Will Smith aliyoicheza yeye (Jaden Smith)
pamoja na Jackie Chan, filamu inaitwa The Karate Kid Drama, kuna kitu
kikubwa sana kinachohusu mafanikio nilichojifunza ndani ya filamu hiyo
ambayo ni ngumu kuisahau. Baada ya Jaden Smith kuonekana hafai na tena
ni mdhaifu katikati ya adui zake ambao ni watoto wenye asili ya kichina,
hata ikafikia kuwahofia kila anapokutana nao kwa sababu ya uwezo na
nguvu walizokuwanazo katika kupigana karate. Hii ilimfanya Jaden kuwa
mnyonge na hata kuamua kutafuta shule na mwalimu mzuri wa kumfunza namna
ya kupigana na kuwa imara katika mchezo wa karate. Ukweli ni kwamba
baada ya Jaden kuamua kurudi upya na kukaa chini ya mwalimu wake Jackie
Chan na kufundishwa namna kamili ya kupigana, alijikuta anafanikiwa
kuwashinda adui zake wote katika mechi ya mwisho aliyoicheza.
Jambo hili ni wazi na halisi katika maisha yetu ya kila siku hapa
duniani. Haupaswi kukata tamaa na kuangalia ni wapi umeshindwa au
kudharaulika, bali unachotakiwa ni kuangalia ndoto yako na ushindi
unaoutaka katika maisha yako. Hata kama watu wakikudharau na kukucheka
leo kutokana na kiwango chako kidogo cha upeo ulichonacho, mwamini Mungu
na amini katika uwezo wako aliokupa, amua kujifunza na kutafuta kujua
namna ya kuweza kufanikiwa na kuelekea katika kilele cha mafanikio yako.
3: Watu wanaoanzia chini ni ngumu kupoteza mafanikio yao.
Kama utaamua kuanzia chini au hapo ulipo, hautokuwa na chochote cha
kupoteza kwa hapo badae. Wakati unaonekana ni mtu wa hali ya chini au
haufai kwa watu waliokuzunguka, basi ni vizuri kuamini katika uwezo wako
na kuamua kuangalia ni wapi unapotaka kufika, hii ni moja ya njia nzuri
ya kuweza kukusaidia kutimiza malengo na ndoto zako kwa haraka zaidi.
Mara nyingi watu wengi inapotokea wanasemwa kidogo tu na watu wa karibu
yao, huwa wanafikia kukata tamaa hata kushindwa kuendelea mbele dhidi ya
kutafuta ushindi wanaoutarajia. Kujishusha na kuamua kudharaulika eneo
fulani kwa kipindi kifupi, nafasi hii itakupa nguvu na uwezo wa
kujifunza mambo mengi zaidi, ambayo kwa hayo utakuwa umeamua kujijengea
ndani yako misuli ya imani na mafanikio dhidi ya kule unapoelekea.
“Look for the person everyone hates, and love them.”
―Criss Jami
Hauhitaji kusubiri watu wakuthibitishie uwezo wako mkubwa ulionao
ndani yako, kisha uanze kuchukua hatua dhidi ya ndoto yako. Hauhitaji
kumwomba mtu yoyote ruksa ya kutimiza maono na picha uliyonayo ndani
yako; unahitaji kuweka malengo na vipaumbele vyako muhimu ili uweze
kuchukua hatua kila siku katika kuhakikisha unafanikiwa. Kwa mfano, kama
unafanya biashara yenye kipato cha hali ya chini na unatamani
kufanikiwa na kufungua biashara nyingine, amini unaweza kufanya hivyo
kama utaamua kujiamini na kujikubali kuwa unaweza.
Post a Comment
Click to see the code!
To insert emoticon you must added at least one space before the code.