0

HOSPITALI YA RUFANI YA MKOA WA DODOMA.

HOSPITALI ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma, inadaiwa zaidi ya Sh. milioni 140 na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (Duwasa), ikiwa malimbikizo ya deni la majisafi na majitaka.
Hayo yalibainishwa juzi na Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Nassoro Mzee, alipokuwa akitoa taarifa mbalimbali na changamoto za hospitali hiyo kwa Naibu Waziri wa Nchi wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina, alipofanya ziara katika hospitali hiyo.

Alisema hospitali inadai zaidi ya Sh. milioni 140 kutokana na huduma za majisafi na majitaka zinazotolewa na Duwasa. Alisema deni hilo ni malimbikzo ya muda mrefu na kwamba kila mwezi inadaiwa wastani wa Sh. milioni 20.

Mbali na deni hilo, Dk. Mzee alisema hospitali hiyo ina shimo la kuchomera taka ambalo kutokana na mahitaji ya sasa halikidhi viwango.

“Incinerator (tanuru la kuchomea taka) tunayoitumia sasa haina ubora. Haichomi vizuri kuna baadhi ya vifaa ambavyo vinatakiwa kuchomwa na kuyeyushwa kama sindano na vitu vingine, hali hii inatulazimu tuchimbe shimo kuvifukia,” alisema.

Akizungumza baada ya kutembelea hospitali hiyo na kupokea taarifa hiyo, Mpina aliagiza kuhakikisha suala la ujenzi wa tanuru jipya linapewa kipaumbele katika bajeti ijayo.

“Ili kulinda mazingira na kutunza taka hatarishi, lazima mhakikishe hadi Julai Mosi, mwakani, mnakuwa na ‘incinerator’ mpya kwa sjili ya uchomaji wa taka hatarishi katika hospitali yenu,” alisema.

Aidha, Mpina alimwagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi, kuhakikisha usafi wa mazingira unafanyika katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwatoza faini watu ambao wamekuwa wakitupa taka ovyo katika maeneo yasiyostahili.

Source: Nipashe

Post a Comment

 
Top