Abdul-Razaq Badru, Mkurugenzi wa HESLB |
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya juu (HESLB), imetangaza mpango
wa kupitia upya na kusitisha mikopo wanafunzi wote inaodai kuwa walipewa
mikopo lakini hawakidhi vigezo vipya vya utolewaji wa mikopo hiyo,
anaadika Charles William.
Abdul-Razaq Badru, mkurugenzi wa HESLB akizungumza katika ukumbi wa
Idara ya Habari – MAELEZO jijini Dar es Salaam amewambia waandishi wa
habari kuwa bodi hiyo lazima ipitie upya majina ya wanafunzi waliopewa
mikopo hata kama wapo katika mwaka wao wa mwisho wa masomo.
Badru ametaja wanafunzi wanaostahili kupata mikopo kuwa ni yatima,
walemavu au wenye wazazi wasiojiweza pamoja na wale wanaosoma masomo
ambayo ni miongoni mwa vipaumbele vya taifa.
“Kwa vigezo hivi, muombaji anayesoma fani za sayansi za tiba na afya,
ualimu wa Sayansi na Hisabati, uhandisi (Viwanda, Kilimo, Mifugo Mafuta
na Gesi) au yatima, mlemavu na mwenye wazazi wenye hali duni au
wasiojiweza ndiye anayestahili kupata mkopo.
HESLB tutahakiki upya wanufaikaji wa mikopo waliopo mwaka wa pili, tatu
na hata wale wa mwaka wa nne ili kuondoa kila asiye na sifa na kwa wale
wa mwaka wa kwanza waliokosa mikopo na wanadhani wanazo sifa wakate
rufaa kuanzia Novemba Mosi,” amesema Badru.
Wakati HESLB ikijiandaa kufanya hivyo, Kilonzo Mringo, Rais wa Serikali
ya wanafunzi ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFMSO) amesema iwapo bodi
ya mikopo itafanya hivyo, wanafunzi wengi watashindwa kuendelea na
masomo.
“Mpaka sasa IFM wanafunzi wengi wana sifa na wamenyimwa mikopo, wengine
wameamua kusitisha masomo yao na wengine wanasoma kwa kuja chuo wiki
moja, nyingine wanaenda kutafuta fedha. Hali ni mbaya, wakiamua
kupunguza tena idadi ya wanaopata mikopo basi chuo kitabaki kitupu,”
amesema Mringo.
Eliudi Kasunzu, Waziri wa Mikopo katika Serikali ya Wanafunzi wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO) ameiambia MwanaHALISI Online kuwa
hawapingi zoezi la uhakiki lakini wanaishangaa HESLB kuhakiki wanaopata
mikopo ambao ni wachache na kuacha kuhakiki wengi walionyimwa.
“Hatuoni mantiki ya kutuhakiki tena kwa kuleta dodoso wanafunzi wajaze,
fomu za maombi wanazo huko ofisini kwao wakihitaji kuhakiki basi
waziangalie na si kutuingiza kwenye usumbufu wa kujaza dodoso wakati
hivi karibuni wamefanya uhakiki wa idadi ya wanufaikaji.
“Hata vigezo walivyoweka mwanzo hawazingatii, tuna orodha kubwa ya
wanafunzi yatima, walemavu na wanaosoma masomo yanayotajwa kuwa ni
vipaumbele vya taifa lakini bado wamenyimwa mkopo halafu wanataka
wachache waliopata wawapunguze zaidi,” amesema.
Boniface Emmanuel, Waziri Mkuu wa DARUSO yeye amesema anadhani kitendo
cha HESLB kutaka kuhakiki wanafunzi wanaoendelea na masomo ni mbinu ya
kuchelewesha kuwapa fedha zao za kujikimu.
“Kama mtu aliomba mkopo mwaka mmoja, miwili au mitatu iliyopita na
akaonekana kwa bajeti na uchambuzi wa wakati huo ana vigezo vya kupata
mkopo, iweje umuhakiki mwaka huu? Nadhani wanatafuta kisingizio cha
kuchelewa kulipa fedha za kujikimu za awamu zijazo kwa kisingizio cha
uhakiki,” amesema Boniface.
Post a Comment