Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita leo amekiri kuwa mtangulizi wake ambaye amefariki dunia, Didas Masaburi alifanya kazi kubwa ya kuboresha miundombinu ya jiji hilo pamoja na kulitambulisha katika anga za kimataifa.
Meya Mwita ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam katika safari ya mwisho ya kuuaga mwili wa Marehemu Masaburi aliyefariki dunia usiku wa kuamkia Alhamisi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Binadamu anapokuwa ameondoka huwa tunazungumza mema aliyoyafanya katika jamii yetu. Mimi Sikuwahi kufanya nae kazi lakini nimekuta kazi ambazo amefanya katika halmashauri ya jiji,” amesema.
Ameongeza kuwa “Moja ya mambo ambayo sitasahau niliyoyakuta aliyoyafanya katika utawala wake ni kuuleta mradi wa DMDP uliolenga kusukuma na kutaka kuboresha maeneo ya miundombinu ya DSM, ukiona kazi aliyoacha mimi ndio naendelea nayo sasa.”
Amesema jambo lingine alilofanya Marehemu Masaburi enzi za utawala wake ni kuleta miji mikubwa duniani kuja kuwekeza na kutoa misaada ya kimaendeleo nchini.
Miongoni mwa majiji aliyoyataja Mwita ni jiji la Hamburg, Shanghai na Torotonto.
“Aliileta hapa miji mikubwa duniani, mimi napata mialiko sasa katika nchi mbalimbali na hii ni matunda ya jitihada zake katika kulitangaza jiji la Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla.” amesema.
Pia Meya Mwita amesema kuwa, Masaburi alifanikiwa kutoa mamlaka na madaraka ya kiutendaji kutoka serikali kuu hadi serikali za mitaa.
“Alipokuwa akiongolea dhana kubwa ya kutoa madaraka kutoka serikali kuu kuja serikali za mitaahili, alikuwa anamaanisha. Jambo hili si jepesi kwa kuwa, halmashauri za mitaa bila ya kuwa na nguvu kubwa haziwezi leta maendeleo mfano Kenya na Uganda halmashauri zake zinauwezo na mamlaka ya kupanga maendeleo,” amesema.
Amesisitiza kuwa “Japo hakufanikiwa kwa kiwango hicho mawazo yake yataishi na mimi kama mrithi wake nitaendelea kuyaenzi.”
Marehemu Didas Masaburi enzi za uhai wake aliwahi kuwa Diwani wa Kata ya Kivukoni, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Serikali za Mitaa (ALAT).
Post a Comment