0

MAOFISA watatu wa Benki ya Maendeleo (TIB) wamepandishwa kizimbani, wakikabiliwa na mashitaka ya kuomba na kupokea rushwa ya Sh milioni tano ili kumsaidia mteja apate hati ya nyumba, iliyokuwa inashikiliwa na benki hiyo, kama dhamana ya mkopo.

Washitakiwa hao ambao ni maofisa Ufilisi wa benki hiyo, Edward Sizya, Aloyce Lufungulo na Karani, Salum Salum, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam. Walisomewa mashtaka manne na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Odessa Horombe mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage.

Odessa alidai Oktoba mwaka huu katika ofisi za TIB Tawi la Upanga, zilizopo Ilala, Dar es Salaam, wakiwa maofisa Ufilisi wa benki hiyo na karani waliomba hongo ya Sh milioni tano kwa manufaa yao binafsi.

Ilidaiwa waliomba fedha hizo kutoka kwa Gosbert Matale, kama kishawishi kumsaidia Evelina Mdecha kukomboa hati ya nyumba inayoshikiliwa na benki hiyo, kama dhamana ya mkopo.

Wakili huyo alidai kuwa Septemba mwaka huu katika ofisi hizo, Sizya akiwa mwajiriwa wa benki hiyo aliomba Sh milioni tano kutoka kwa Evelina, kama kishawishi kumsaidia kukomboa hati yake ya nyumba inayoshikiliwa na benki hiyo na inadaiwa Oktoba 12, mwaka huu, katika ofisi hizo, Sizya alikubali kupokea Sh milioni mbili kutoka kwa Evelina ili amsaidie kupata hati hiyo.

Katika mashtaka mengine, Sizya anadaiwa Oktoba 18, mwaka huu, katika ofisi hizo kwa manufaa yake alipokea Sh 200,000 kutoka kwa Evelina, kama kishawishi cha kumsaidia kukomboa hati hiyo. Washtakiwa walikana mashitaka na Wakili Odessa alidai upelelezi haujakamilika. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 8 mwaka huu itakapotajwa tena.

Post a Comment

 
Top