0
Tokeo la picha la watumishi
SERIKALI imesema uhakiki wa watumishi wa umma, utakamilika ndani ya mwezi huu, hivyo nafasi zilizoachwa wazi baada ya kuondolewa kwa watumishi hewa, zitaanza kujazwa.
Aidha, imesema kwamba baada ya uhakiki huo ambao utasaidia kuwa na orodha sahihi ya watumishi waliopo katika taasisi za umma kwa lengo la kuboresha hali ya utumishi nchini, itaanza mfumo wa kuhakiki majina mapya.
Akizungumza katika awamu ya pili ya kipindi cha Tunatekeleza kinachorushwa TBC 1 juzi, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro alisema uhakiki wa watumishi hewa, umesaidia kuongeza ufanisi katika taasisi zake.
Dk Ndumbaro alisema baada ya kukamilika kwa uhakiki huo, pia wataanza mfumo mwingine wa kuhakiki majina mapya ambayo yatajitokeza mara mbili na kuyatoa ili kubaki na majina sahihi.
“Kwa mfano, yupo mtu anatumia majina matatu lakini akatokea mmoja akaondoa lile la katikati na kubaki na majina mawili labda Laurean Ndumbaro hivyo mfumo utaona kuwa ni jina jipya kumbe kuna mtu ambaye amejitengenezea jina hilo,” alisema Dk Ndumbaro na kufafanua kuwa ili kuondoa mkanganyiko huo, mfumo utatambua na kuyaondoa majina yasiyohusika.
Pia alisema mfumo wa usajili kupitia Vitambulisho vya Taifa (NIDA), utasaidia kwa kiasi kikubwa, kwani utatoa taarifa sahihi za watumishi halali wa serikali.
Aidha, alisema Serikali ya Awamu ya Tano imetia mkazo katika uadilifu na kwamba kauli ya Rais John Magufuli inatekelezwa ipasavyo na watumishi wa umma.
Alisisitiza kuwa kwa ujumla hali ya utumishi wa umma imeimarika tofauti na ilivyokuwa zamani na kwamba wataendelea kuwachukulia hatua watumishi watakaokiuka maadili.
“Kauli ya Rais ya ‘Hapa Kazi Tu’ inatekelezwa vizuri katika utumishi wa umma. Majukumu yetu ni kuandaa na kusimamia sera, kanuni, taratibu, sheria miundo na miongozo inayohusu rasilimali watu katika watumishi wa umma. Pia jukumu la kusimamia maadili ya utumishi wa umma hasa wale ambao hawaangukii kwenye tume ya maadili ambao sio viongozi wa juu,’’ alifafanua Dk Ndumbaro.
Hata hivyo, alisema ili kutilia mkazo kipaumbele hicho cha uadilifu, serikali imekuwa ikiwafikisha mahakamani na kuwachukulia hatua za kinidhamu, watumishi ambao wanakiuka maadili pamoja na kutoa mafunzo sehemu mbalimbali juu ya maadili ya utumishi wa umma.
Kwa mujibu wa Dk Ndumbaro, katika tathmini waliyoifanya imebaini kuwa yapo maeneo yameonesha kuwa viwango vya maadili viko chini ikiwemo maeneo ya fedha na sekta zinazowagusa wananchi moja kwa moja.
Alisema baada ya tathmini hiyo, wanatilia mkazo kwa wafanyakazi kuzingatia kanuni za uadilifu na kuona umuhimu wa kuzingatia taratibu na miongozo ya utumishi na kwamba kwa wale wanaokiuka huchukuliwa hatua za kinidhamu, kushushwa vyeo pamoja na mshahara.
‘’Zamani watumishi waliokuwa wakifanya vibaya ndio waliokuwa wanapewa motisha lakini kwa waliokuwa wanafanya vizuri walikuwa wakiulizwa wamewezaje kufanya hivyo. Kwa hiyo, sisi tunatambua watumishi wanaofanya kazi vizuri kwamba kunalipa,’’ alisema.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu katika wizara hiyo, Suzan Mlay alikiri kwamba kulikuwa na malalamiko ya utendaji usioridhisha wa utumishi wa umma lakini wanawasisitiza watumishi umuhimu wa kuzingatia maadili kutoa huduma kwa wananchi kwa haraka na kadri ya uwezo wake.
“Kipindi kifupi baada ya miezi mitatu iliyopita tumepata mrejesho kutoka kwa wafanyakazi, wastaafu watumishi na wadau mbalimbali ambao wanakuja maofisini na wanasema hali ya utumishi imebadilika kuliko ilivyokuwa zamani,’’ alisema Mlay.

Post a Comment

 
Top