0


KUNA kitu kimoja hujakisikia. Jana Jumatatu Mwenyekiti wa Yanga,Yusuf Manji aliwaita ghafla wachezaji wote kwenye ofisi zake za Quality Plaza Jijini Dar es Salaam na kufanya nao kikao cha faragha ambacho hakuna aliyeruhusiwa kujua ajenda kuu zaidi ya wahusika. Lakini baadae ikabainika kwamba alikuwa akiwajaza mzuka kuelekea kwenye mechi ya Ndanda kesho. Kingine ni kwamba straika Mzambia, Obrey Chirwa hatimaye amefunga bao kwenye mechi ya kirafiki na kuondoa gundu, alitupia kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Yanga B iliyopigwa Ijumaa kwenye Uwanja wa Gymkhana ambao upo pembezoni kidogo kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Chirwa alitupia goli la kwanza na lile la pili akafunga Donald Ngoma, Yanga wametafsiri bao Chirwa kuwa ni kuondoa gundu na huenda kuanzia mechi za kesho Jumatano kwenye Ligi Kuu Bara akaanza kucheka na nyavu.

Simba kama itaifunga Ruvu Shooting ya Pwani kesho Jumatano kwa mabao mawili ama zaidi itapanda kileleni mwa msimamo wa Ligi wakati ambapo wapinzani wao wakubwa Yanga hata wakiifunga Ndanda mabao kumi kwa bila bado italazimika kusubiri kwa muda mrefu ili kuweza kushikilia usukani wa Ligi hiyo.

Simba mpaka sasa ina pointi nne na inashika nafasi ya tano wakati Mbeya City inaongoza ligi ikiwa na pointi saba ambazo Simba ikishinda ikazifikia lakini inahitaji mabao zaidi ya mawili ili kuipiku Mbeya City kila idara na kushikilia usukani huo.

Yanga ambayo imecheza mechi moja tu msimu huu ina pointi tatu na imejikita katika nafasi ya nane ambapo kama itashinda kesho itaweza kupanda hadi nafasi ya pili hadi ya nne ambayo hayo yatatokana pia na matokeo ya mchezo kati ya Prisons ya Mbeya na Azam FC.

Kocha wa Yanga, Hans Van Pluijm alisema anakwenda Mtwara kwa tahadhari hasa kutokana na ukweli kwamba atawakosa wachezaji wake wawili beki Vincent Bossou na kiungo Haruna Niyonzima ambao walikwenda kuzitumikia timu zao za taifa na hawataweza kurejea kwa wakati.

“Niliitazama Ndanda ilivyocheza na Simba, siyo timu ya kubeza kwani ina kikosi imara, ubaya kwetu ni kwamba tunakwenda katika mchezo huo tukiwakosa baadhi ya wachezaji wetu, hata hivyo tutapambana,” alisema Pluijm.

Simba kwa upande wake itacheza na Ruvu Shooting ambayo imeanza msimu huu vizuri kwa kushinda mchezo mmoja na kupata sare katika mchezo mwingine na kujikita katika nafasi ya saba na pointi nne.

Post a Comment

 
Top