0
RAIS John Magufuli leo anatarajia kuzindua ndege mbili, zilizonunuliwa na serikali kwa ajili ya kuwahudumia wananchi, ikiwa ni moja ya utekelezaji wa ahadi zake za kulifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Ndege ya pili iliwasili jana septemba 27 baada ya ile ya kwanza kuwasili nchini Septemba 20 mwaka huu. Ndege zote zina uwezo wa kubeba watu 76 kwa kila moja.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, anayeshughulikia Uchukuzi, Dk Leonard Chamuriho, alisema uzinduzi huo utafanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal 1).
“Ndege hizi mbili aina ya Dash 8 Q400 zimetengenezwa na kiwanda cha Bombardier nchini Canada na zitahudumia soko la ndani na nchi jirani,” alisema.
Chamuriho aliwakaribisha wananchi wote kushuhudia uzinduzi huo wa ndege, unaotarajiwa kuanza saa 2.00 asubuhi ili kujionea utekelezaji wa ahadi za Serikali katika mkakati wa kuhuisha usafiri wa anga nchini.
Ndege hizo zitakuwa na madaraja mawili yaani daraja la uchumi, litakalohusisha abiria 70 na daraja la biashara litakalohusisha abiria sita kwa kila ndege.

Post a Comment

 
Top