Karibu tena ndugu na rafiki yangu katika wakati mwingine wa
Kuelimishana katika eneo maalumu la ujasiriamali na biashara. Leo nataka
tuangazie mambo sita muhimu yanayoweza kukusaidia kama mfanyabiashara
katika kuifanya biashara yako kuendelea kuishi. Ninaposema biashara
kuendelea kuishi, nina maana ya kuendelea kuishi kweli kweli na si nje
ya hapo; kwani kila biashara uzaliwa, ukua na wakati mwingine inaweza
kufa pale ambapo tu mwenye nayo hatokuwa mwangalifu katika kuilea na
kuzingatia kanuni za kuikuza na kuindeleza kwa ufanisi.
Zipo biashara nyingi zilizoazishwa na badae kufa kwa muda mfupi baada
ya kuanzishwa na badae kutokana na kukosa usimamizi mzuri na wakutosha
zikasababisha kuanguka na kufa moja kwa moja. Wewe mwenyewe ni shahidi
yawezekana unafahamu baadhi ya biashara zilizokumbwa na tatizo hili, na
kushindwa kufikia hatua ya juu ya mafanikio na malengo yake. Yapo
makampuni binafsi na hata ya kiserikali yalipokosa usimamizi mzuri na
wakutosha yalikufa na hadi leo yamepotea na kubaki kuwa historia tu.
Je, unazani ni nini kinachosababisha kampuni na biashara nyingi
kuanguka na kufa kwa muda mfupi? Hili ndio swali linaloleta majibu sita
ambayo yanazaa makala hii na mafundisho haya ya wazi kwa njia ya mtandao
siku ya leo. Nimekuandalia kwa ufupi mambo sita ambayo yanaweza
kuisadia kampuni yako kuishi, na kuzuia kuanguka; lakini katika mambo
haya sita tambua usipoyafanya na kuyazingatia yanaweza kusababisha
biashara au kampuni yako kufa na kutokufikia katika mafanikio makubwa
unayoyahitaji katika biashara yako.
Jambo la Kwanza:
Kuwa na Maono halisi ya Unachokitaka.
Biashara yoyote ile inahitaji kuwa na maono na picha halisi ya kile
inachokifanya katika soko lake, iwe ni katika soko la bidhaa au huduma.
Ni vyema kila mtu asimamie maono na melengo makuu ya kuanzisha biashara
yake aliyonayo. Yawezekana una biashara au hauna biashara lakini nataka
uzingatie kanuni kuu ya kutazamia unachokifanya au ulicholenga kukifanya
dhidi ya wateja wako sokoni.
Maono ni muhimu sana katika kuiongoza biashara yoyote ile katika
kufikia mafanikio na malengo yake makubwa iliyojiwekea. Kama unahitaji
biashara yako iwe sehemu ya kuendelea kuishi na kubaki sokoni ni vizuri
uzingatie maono halisi yaliyokufanya uanzishe biashara yako uliyonayo
sasa.
Jambo la Pili:
Jitoe Kikamilifu katika Biashara yako.
Nataka nikuongezee jambo hili; kumbuka kwamba kujitoa kunaenda na
kupenda. Hivyo kama unataka kuendelea kubaki sokoni na kuwa kinara
katika kulitawala soko ni vizuri ujitoe kikamilifu katika kuijali na
kuipenda biashara yako unayoifanya siku zote. Huwezi kufanikiwa katika
biashara yako kama wewe binafsi hutaki kutoa nafasi ya kupenda kile
unachokifanya.
Jifunze kujitoa na kupenda kile kitu unachokifanya. Kwa kufanya hivyo
utajisaidia binafsi kuwa na nidhamu ya kufanya biashara yako au kitu
hicho pasipo kukata tamaa hata pale inapofikia kutokwenda vizuri kimauzo
na masoko. Biashara ni kama mtoto anayehitaji malezi mema ili akue
vizuri na kufikia hatua njema ya kujitegemea.
Jambo la Tatu:
Tambua Hasara (Risk) ni sehemu ya biashara.
Unashangaa kusikia jambo la namna hiyo. Nataka nikuambie kuwa;
mfanyabishara makini huwa hakimbii wala haogopi hasara zinazotokea
katika biashara yake, bali anatafuta namna ya kukabiliana na hasara hizo
pale zinapojitokeza. Kikubwa ni kuangalia ukubwa na kiwango cha hasara
inayotokea isizidi uwezo wote wa biashara. Kuna hasara (Risk) ambazo
kila biashara kwa sehemu yake inaweza kuziendesha na kuziepuka (Manage
and Control Risk).
Angalia husiwe mwoga unapokutana na hasara ndogo kwa kuhofia
kuanguka, bali fahamu namna ya kuziendesha na kuziepuka hasara hizo ili
uweze kufikia mafanikio makubwa katika biashara yako na kuifanya
biashara yako kuendelea kuishi.
Jambo la Nne:
Kuwa Mwenye shauku zaidi.
Kama hauna shauku ya kufanikiwa basi hautoweza kuisaidia biashara
yako kukua, bali utakuwa sababu kubwa ya biashara yako kufa. Matamanio
ya Mafanikio kwa ajili yako binafsi na biashara yako ni ya muhimu sana
katika kukupa msukumo wa ndani wa kujituma na kufanya kazi kwa bidii,
ili uweze kufikia mafanikio makubwa kwa ajili yako binafsi na biashara
yako.
Jifunze kuwa na shauku kamili ya kutimiza maono na malengo yako
uliyonayo katika biashara na kwako binafsi; hii itakujengea kujituma,
kutokukata tamaa na kujikubali binafsi katika kile unachokifanya. Kwa
kufanya hivyo utakuwa na nguvu ya kuitumikia biashara yako kwa moyo wako
wote na kuwa sababu ya kuzuia anguko na kufa kwa biashara yako.
Jambo la Tano:
Fanya Mpango-Biashara (Business Plan) kuwa kiongozi wako.
Hapa ninaongea na wewe unayefanya biashara au kumiliki kampuni iliyo
na mipango muhimu na maalum kwa ajili ya miaka mitano, kumi, ishirini
hadi maisha. Ni muhimu kutumia mpango biashara wako ulionao kama
mwongozo katika kukusaidia kuiendesha na kuiendeleza biashara au kampuni
yako hadi kwenye mafanikio makubwa unayoyahitaji wewe binafsi, kama
mbeba maono wa biashara au kampuni husika.
Ndio maana kuna umuhimu kila kampuni au mmiliki wa biashara kufahamu
umuhimu wa kuwa na mpango biashara wa kampuni au biashara yake, ili
kumsaidia na kumwongoza katika mafanikio makubwa ya kutimiza maono na
malengo ya kampuni yake husika.
Jambo la Sita:
Kubali mabadiliko yanayojitokeza.
Ninapozungumzia suala la mabadiliko fahamu ninazungumzia suala zima
la kukubaliana na ujio wa teknolojia na hali ya mfumo mzima wa
kukabiliana na ushindani mkubwa wa kuwepo kwa taarifa nyingi,
zinazoongeza watu kufanya kazi usiku na mchana ili kukubiliana na soko
la dunia ya leo. Usipokubali kuenenda na mfumo huu, uwe na uhakika
utashindwa kufanikiwa katika biashara na utakuwa sababu ya kuiua
biashara yako kirahisi.
Usikimbie mabadiliko ya kiteknolojia katika ufanyaji wa kazi katika
biashara yako; bali tafuta namna bora ya kuendana nayo ili uweze
kushindana katika soko na kuifanya biashara yako iendelee kuishi na
kusonga mbele zaidi. Nataka nikuambie kwa dunia ya sasa ushindani wa
kibiashara umeongezeka na utaendelea kuongezeka ukichangiwa kwa sehemu
kubwa na ongezeko la kuwepo kwa teknolojia na taarifa nyingi duniani.
Hivyo hutakiwi kuwa nyuma katika hilo na kusema hutaki kuendana na hali
hiyo inayojitokeza; fahamu kwa kufanya hivyo kwa sehemu kubwa utaua
biashara au kampuni yako.
Hadi kufikia hapo nakutaka uchukue hatua ya kutekeleza yale yote
uliyojifunza katika makala hii, ili uweze kuifanya biashara yako
kuendelea kuishi na kuzuia anguko la kufa na kupotea katika soko. Hadi
siku nyingine tutakapokutana tena kwa makala nyingine nzuri zaidi za
biashara na ujasiriamali; nikutakie siku njema na mafanikio mema katika
biashara yako.
Post a Comment