0

OFISI ya Makamu wa Rais imetoa miezi minne kuanzia Agosti 18, mwaka huu kwa wamiliki wa viwanda vyote vinavyozalisha mifuko ya plastiki nchini kuchukua hatua stahiki kusitisha uzalishaji wa mifuko ya plastiki na kuwekeza katika mifuko mbadala na urejeleshaji wa taka za plastiki.

Hatua hiyo imetokana na nia ya serikali kupiga marufuku matumizi ya mifuko hiyo ifikapo Januari 1,mwaka 2017.

Taarifa kwa umma iliyotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais imeeleza kuwa upigaji marufuku matumizi hayo unajumuisha uingizaji, uzalishaji, uuzaji na utumiaji wa mifuko kama vifungashio vya maji na bidhaa zingine. Ilieleza kuwa azma ya serikali ni kuepusha athari za kiafya na mazingira zinazoendelea kujitokeza kutokana na matumizi ya mifuko hiyo.

“Athari hizo ni pamoja na mifuko hiyo kutooza hivyo kuathiri udongo, kuzagaa katika sehemu mbalimbali, kuziba miundombinu ya majitaka na mifereji ya mvua na kusababisha mafuriko, kuharibu mfumo wa ikolojia na bayoanuai,”ilisema taarifa hiyo.

Mifuko hiyo pia husababisha vifo kwa wanyama wanapoimeza, kuhatarisha afya ya binadamu kutokana na kutumika kufungashia vyakula hususan vya moto, inapotumia kuwashia mkaa majumbani wakati wa kupika na uchafuzi wa hewa zinapoungua.

Post a Comment

 
Top