WIZARA
ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema itafuatilia malalamiko kuhusu kitendo
cha kufungwa wakati wa usiku kwa baadhi ya vituo vikubwa vya Polisi
jijini Dar es Salaam, hatua inayosababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi.
Hayo
yalisemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf
Masauni alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
Masauni
alisema wizara hiyo itafanya ukaguzi wa kina ili kubaini kama vipo
vituo vya Polisi, vinavyopaswa kuwa wazi wakati wa usiku, lakini badala
yake vinafungwa na kufanya wananchi kushindwa kupata huduma. Masauni
alisema vituo vya Polisi vinapaswa kufanya kazi muda wote hata wakati wa
usiku, isipokuwa Vituo Daraja C pekee, ndivyo vinapaswa kufungwa
nyakati za usiku.
Alisema
vituo vyenye Daraja A na B, vinapaswa kufanya kazi muda wote, hivyo
endapo kuna vituo vyenye madaraja hayo vinafungwa vinakwenda kinyume
hivyo atafuatilia ili kubaini vituo hivyo.
Vituo
vya Polisi vya Daraja A na Daraja B ni vile ambavyo vinajengwa katika
Makao Makuu ya Wilaya na Mikoa ya Kipolisi na katika miji inayokua,
wakati Vituo vya Daraja C ni vituo vidogo maarufu kama Polisi Posti.
Katika
kukabiliana na vitendo vya uvamizi katika vituo vya Polisi na kupora
silaha, Jeshi la Polisi lilitangaza kufungwa kwa vituo vidogo vya Polisi
ifikapo saa 12 jioni.
Hata
hivyo, uchunguzi wa gazeti hili umebaini vituo vikubwa vya Daraja B
kikiwemo Kituo cha Polisi cha Tabata jijini Dar es Salaam, vimekuwa
vikifungwa usiku na wananchi kulazimishwa kueleza shida zao nje ya kituo
na baadaye kuamriwa kurejea asubuhi bila kupewa msaada.
Akizungumzia
suala hilo, Masauni alisema; “Taratibu zinafahamika kwa madaraja A na B
kufanya kazi muda wote na Daraja C pekee ndivyo vinapaswa kufungwa,
nitafuatilia ili kubaini vituo hivyo ili tuweze kuchukua hatua.”
|
Post a Comment