MAMLAKA
ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA) imeainisha mikakati yake ya kufanya
maboresho katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)
kwa kuboresha jengo la abiria (terminal II), ambayo yataenda sambamba na
ujenzi wa terminal III.
Aidha,
imesema iko kwenye mchakato wa kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya
ujenzi wa njia ya kurukia ndege. Pia, imepanga kuoanisha mifumo ya
mawasiliano na usalama katika majengo matatu ya abiria ya uwanja huo
(terminal I, II, III).
Hayo
yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Ramadhan Maleta wakati
akizungumza na viongozi wa dini na wajumbe wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa
Dar es Salaam, waliotembelea ujenzi wa mradi huo wa jengo hilo. Maleta
alisema maboresho ya jengo la terminal II, yataanza mwakani na kwamba
kwa sasa Serikali iko katika mchakato wa kutafuta pesa kwa ajili ya
kufanya maboresho hayo.
“Tunataka
kujenga njia nyingine ya kurukia ndege, kwa sababu wataalamu walifanya
utafiti wakasema kwamba kufikia mwaka 2025, barabara hii moja ya sasa
haitatosha kwa matumizi,” alisema Maleta.
Awali,
akizungumza kwenye ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Shehe wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum alisema mradi huo kama
utakamilika kwa wakati, utawasaidia Watanzania na pia utaongeza idadi ya
ndege kubwa kutua nchini.
Alisema
ujenzi wa jengo hilo ni ishara tosha kuwa Serikali inafanya kazi kubwa
ya kuwaletea wananchi wake maendeleo na kwamba kamati hiyo itashirikiana
na Serikali si tu katika kuhamasisha masuala ya amani bali hata
maendeleo.
“Mradi
huu si tu utawasaidia Watanzania, lakini pia utaleta heshima kwa nchi
kwa kuwa na viwanja vinavyoendana na hadhi ya Watanzania. Sisi tunaunga
mkono juhudi za Serikali kuwaletea maendeleo wananchi,” alisema Shehe
Alhad.
Katibu
wa Kamati hiyo, Padri John Solomon alisema kikubwa kilichowafanya
kutembelea mradi huo ni kutaka kuona juhudi za Serikali, kuhakikisha
Tanzania inakuwa na uwanja mkubwa wa kisasa.
Mbali
na ziara hiyo, kamati hiyo pia ilitumia nafasi hiyo kufanya maombi na
dua kwa ajili ya mradi huo ili uweze kukamilika salama, bila kutokea kwa
tatizo la aina yoyote ambalo linaweza kukwamisha.
Akitoa
ufafanuzi wa mradi huo, Mkurugenzi wa Mradi huo, Mohammed Millanga
alisema, ujenzi wa jengo hilo litakalohudumia abiria milioni sita kwa
mwaka, unatarajiwa kukamilika Desemba mwakani.
Alisema
hadi sasa mradi huo ambao ulikuwa utekelezwe kwa awamu mbili kwa sasa,
awamu hizo zinatekelezwa kwa pamoja na umekamilika kwa asilimia 45.
Hata
hivyo, Millanga alitaja baadhi ya changamoto, kuwa ni maandalizi ya
ufunguzi wa jengo hilo, ambapo alisema wameshaanza kulifanyia kazi jambo
hilo. Changamoto nyingine ni jinsi ya kuoanisha mifumo ya mawasiliano
na usalama katika majengo matatu ya abiria.
“Kitu
kingine ni kwamba wadau walikuwa wanataka mambo mbalimbali, lakini sisi
inabidi tufanye kazi ndani ya bajeti iliyopangwa ili mambo yaweze
kwenda vizuri,” alisema Millanga.
|
Post a Comment