0

Serikali inatarajia kubadilisha sheria za uendeshaji wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) ili kuruhusu sekta binafsi pamoja na serikali ya China kuwekeza ndani ya shirika hilo

hatua hiyo inakuja baada ya kusuasua kiutendaji na kushindwa kufikiwa kwa mafanikio yaliyotarajiwa na serikali juu ya shirika hilo.

Akisisitiza juu ya azma hiyo ya serikali katika maadhimisho ya miaka 40 ya shirika hilo Kaimu Mkurugenzi wa Utathmini na Ufuatiliaji wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Bw. Boniface Meena amesema lengo kuu ni kuliendeleza shirika hilo kiushindani kama yafanyavyo mataifa mengine yaliyoendelea.

“Hatuwezi kuruhusu sekta binafsi kuwekeza bila kubadilisha sheria ya mwaka 1995 inayotaka TAZARA kuendeshwa na serikali pekee, tunaamini sekta binafsi italeta mabadiliko ndani ya TAZARA vivyo hivyo katika barabara, Reli hata Bandari yetu. Tunafanya mabadiliko haya kwalengo la kuhakikisha shuguli za uendeshaji zinakuwa na tija,” amesema Bw. Meena.

Bruno Ching’anu ambaye ni Mkurugenzi wa TAZARA amesema kwa muda wa miezi sita sasa shirika hilo limeweza kutumia siku 4 hadi 7 kufikisha mizigo katika nchi ya Zambia kutoka siku 30 au 35 ambazo walikuwa wakitumia hapo nyuma kuifikisha mizigo Zambia.

“Hatua hii inaamaanisha kweli tuna miaka 40 kwani miaka 40 inatija endapo ulichokusudia kimefanikiwa, tumeboresha maeneo korofi japo tume jiendesha kwa hasara na chini ya kiwango kwa muda mrefu. Hatua za sasa zinatupa nguvu ya kuifikia nchi ya DR. Congo,” amesema Bw. Ching'anu.
Shirika hilo linaendelea na kufufua treni kadhaa kwa ajili ya kuboresha usafirishaji kwa njia ya reli huku lengo kubwa la shirika hilo nikuweza kusafirisha mizigo mpaka nchi ya DR Congo.

Post a Comment

 
Top