0

Septemba mosi mwaka huu inataraji kuingia katika historia ya Tanzania kutokana na matukio ambayo yanataraji kufanyika siku hiyo, matukio hayo ni pamoja na sherehe za miaka 52 ya Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ), maandamano ambayo yamepangwa kufanywa ya UKUTA na tukio la kupatwa kwa jua.

Akizungumza na Waandishi wa Habari wakati alipokutana na Maafisa wa Jeshi la JWTZ Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema JWTZ inapotimiza miaka 52 ni fahari kubwa hivyo tunapaswa kuwapongeza kwa kudumisha amani na mshikamano.

Alisema Jeshi hilo limejipanga kurusha angani ndege zake za kivita katika anga la Dar es Salaam, Septemba 1 mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 52 ya kuanzishwa kwake.

Makonda aliwataka wananchi kutokuwa na hofu wanaposikia ngurumo za ndege hizo bali wafurahie kwani ni ndege zao.

“Mnaposikia milio ya ndege zetu mbalimbali, mfurahie kwa sababu hizo ni ndege za wananchi. Usisikie muungurumo ukashtuka. Hakuna jambo lolote lile zaidi ya kuonesha vifaa vyetu na jinsi ambavyo wanajeshi wetu kwa miaka 52 wamaeendelea kuwa imara na vifaa vizuri,” alisema Makonda.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa waliwataka wananchi waliojipanga katika vikundi mbalimbali kuripoti kwa wakuu wao wa wilaya kujiandikisha ili waweze kushiriki pamoja na Jeshi hilo katika zoezi la usafi jijini humo.

Aliwataka wakazi wa mkoa huo pia kujitokeza kuchangia damu katika vituo mbalimbali ambavyo vimeanishwa ili kuunga mkono juhudi za uchangiaji damu zitakazofanywa na wanajeshi wa JWTZ.

“Hii ni sehemu ya amani, tufanye usafi kwa amani. Tujitolee damu zetu kwa amani na mwisho wa siku tuwaenzi na kuwapongeza wanajeshi wetu kwa kazi kubwa wanayoifanya,” Makonda alieleza.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa aliendelea kutoa onyo kwa watu watakaotaka kufanya maandamano yaliyopigwa marufuku ya oparesheni UKUTA akiwataka kutii sheria.

“Mimi ninavyojua UKUTA ni kuwa mtu amefika mwisho wa kufikiri sasa kama watakuwa wamefika mwisho wa kufikiria basi sisi tutawasaidia … watu wapo wanapanga kufanya mambo ya kusaidia jamii wao wanapanga maandamano nawashauri wananchi waungane na Polisi,” alisema Makonda.

Post a Comment

 
Top