1

Cc-U9Z1UIAAOtwx
Maisha si marahisi wakati wote kama wengi wanavyozani hasa pale unapokutana na changamoto mbali mbali zinazoweza kuwa kizuizi kikubwa juu ya jambo lako zuri unalotaka kulitimiza kwa wakati fulani. Kuna wakati unaweza ukawa unatamani kukamilisha wajibu fulani mkubwa mbele yako, ili uweze kufikia hatua ya juu ya kufanikiwa na kuleta matokeo chanya katika maisha yako lakini hali ikawa tofauti na unavyotaka iwe kwa kipindi hicho. Yawezekana unahitaji kuchukua hatua kwa ajili ya kukamilisha malengo na mipango yako mizuri uliyonayo lakini kila unapootaka kufanya hivyo unakosa msukumo na nguvu ya kuchukua hatua husika.
Mambo mengi umeghairisha kwa sababu ya kukosa msukumo binafsi wa kuchukua hatua za kivitendo na hatimaye umeshindwa kuleta matokeo chanya katika maisha yako. Wapo watu wengi kila wanapojaribu kupanga jambo fulani wanapanga vizuri, ila unapofika wakati wa kutaka kuchukua hatua wanakuwa wanakosa msukumo na nguvu ya ndani ya kuwasaidia kutimiza wajibu walionao ili kuleta matokeo na mabadiliko makubwa katika maisha yao. Je, na wewe ni miongoni mwa watu wa namna hii? Soma makala hii ili kuchukua hatua ya mabadiliko yako leo hii.
Hapa kuna mambo 10 yanayoweza kukusaidia ili kuondokana na hali ya namna hiyo.
1: Kubali tatizo.
Jambo la kwanza ili uweze kuondokana na hali ya kuchoka na kutojisikia kuchukua hatua ya kivitendo juu ya malengo na mipango yako uliyonayo ni kuamua kulikubali tatizo. Ndio. Kubali kuwa una tatizo la kutokuchukua hatua za haraka na mara kwa mara kila unapotaka kufanya hivyo, kwani unapokubali tatizo unatoa nafasi ya kulishugulikia hilo tatizo kwa moyo wako wote hadi linaondoka.
2: Tengeneza ratiba na kuifuata kila siku.
Baada ya kukubali una tatizo la kutokuwa na wepesi wa kuchukua hatua ni vizuri utengeneze ratiba yako maalum inayoweza kuwa msaada mkubwa kwako kwa ajili kukupa mwelekeo katika majukumu yako ya kila siku. Unapokuwa na ratiba au unapojiwekea vipaumbele vyako vya kufanya kila siku unakuwa umejifunga mwenyewe binafsi kiakili na kifikra juu ya mambo gani ya kufanya juu ya siku nzima uliyonayo mbele yako.
3: Tengeneza picha ya mafanikio yako unayohitaji.
Unapotengeneza picha halisi juu ya jambo fulani unalotaka kulitimiza hii itakusaidia zaidi kukupa nguvu na msukumo mkubwa ndani yako hasa kwa ajili ya kuchukua hatua za kivitendo pasipo hofu na uoga ndani yako. Jifunze kuona mafanikio ndani yako kabla hayajawa halisi katika hali ya nje hii ndio njia nzuri ya kukupa msukumo wa kipekee wa kutimiza malengo na mipango yako yote uliyonayo.
4: Tafuta namna ya kujihamasisha mwenyewe.
Unapochukua hatua ya kujihamasisha mwenyewe binafsi unakuwa unatengeneza nguvu mpya ndani yako itakayokufanya kupata msukumo wa kuchukua hatua ya haraka ya kivitendo juu ya ndoto yako uliyoanayo. Jifunze kujihamasisha kwa kupitia kusoma vitabu vinavyohusiana na fani yako au kitu unachofanya, sikiliza mafundisho mazuri ya kukujenga na kukupa hatua mpya, penda kuhudhulia semina na warsha mbalimbali za kukujenga na kukusaidia katika kufikia ndoto yako.
5: Weka uzito juu ya jambo unalotaka kulifanya.
Ni vyema usisubiri mtu mwingine aje kwa ajili ya kukusaidia kuona uthamani na uzito wa ndoto yako uliyonayo. Kama unataka kufanikiwa kwenye kila jambo unalotaka kulichukulia hatua za kivitendo na kulifanikisha kwa haraka, ni vizuri ujifunze kuweka uzito kwenye kila jukumu ulilonalo mbele yako pasipo kujiwekea kizuizi cha hofu na mashaka ya kulitekeleza. Fanya hivyo leo ili kuleta matokeo makubwa katika maisha yako. Weka uzito kwenye kila jambo unalolifanya ili kuleta matokeo makubwa yatakayowashangaza watu wengi.
6: Anza na hatua ndogo kwanza.
Wapo watu wengi kila wanapotaka kutimiza malengo yao na mipango fulani waliyonayo huwa ni watu wa kusubiri wafanikishe kwanza hatua fulani kubwa itakayoweza kuwaletea mafanikio ya haraka kabla hawajapita kwenye hatua ndogo zinazoweza kuwa msingi mzuri wa kule wanapoelekea. Anza kidogo kidogo kwa ulichonacho; anza kuchukua hatua ndogo leo hii ili uweze kuleta matokeo madogo yanayoweza kuzaa njia mpya na pana ya kukupeleka katika mafanikio mengine makubwa zaidi.
7: Furahia mafanikio madogo unayoyapata.
Usikubali kuishi ukisubiri ufanikishe kila kitu ndio uwe na furaha ya kutosha maishani mwako. Jifunze kujenga furaha katika kila hatua unayoipiga katika maisha yako, furahia hatua ndogo uliyoipiga katika kufanikisha malengo yako uliyokuwanayo pasipo kusubiri hatua fulani ya kiwango cha juu ili kuleta furaha unayohitaji ndani ya moyo wako. Kumbuka furaha pia ni mojawapo ya chanzo cha mafanikio yako unayohitaji, unapopoteza furaha ndani yako unakuwa unapoteza nguvu ya kusogea mbele.
8: Kubali changamoto na amua kusonga mbele.
Kama umeshindwa kufanikisha lengo lako moja usikubali kukata tamaa ya kuchukua hatua kwenye lengo lako lingine ulilonalo maishani mwako. Amua kukubali kila changamoto unayokutana nayo kwenye maisha yako na kuikabili ili uweze kufanikisha ndoto yako uliyonayo, usikate tamaa haraka kwa sababu hujafanikisha malengo mengine uliyokuwanayo, songa mbele amini kwa bidii na juhudi yako utafanikiwa.
9: Tafuta mshauri wa karibu (mentor).
Unapokuwa na mtu wa kukushauri na kukusaidia kimawazo kila unapopitia hali ngumu ya kukosa hamasiko la kuchukua hatua fulani katika malengo yako, hii ni njia nzuri inayoweza kukuweka salama zaidi hasa katika kukupa mwelekeo mpya na nguvu kubwa ya kusonga mbele kila wakati. Tafuta mtu unayemwamini zaidi na anayeweza kuwa mshauri na mwelekezi mzuri katika maisha yako katika kile kitu unachotaka kukifanikisha (life coach or mentor).
10: Tafuta msaada kutoka kwa wengine.
Kumbuka kila mtu amepewa kipaji chake na uwezo wa kipekee ndani yake unaokuwa tofauti na mwingine. Hivyo basi ni vizuri unapopitia katika hali ya kuchoka au kutokujisikia kuchukua hatua fulani juu ya jambo unalotaka kulifanikisha, ni vyema uamue kutafuta watu waaminifu wa karibu yako kama vile marafiki unaowaamini, ndugu, wazazi, mshauri wako, nakadhalika, ili waweze kukusaidia na kukutia moyo juu ya jambo unalotaka kufanya. Amini unauwezo mkubwa ndani yako, chukua hatua leo pasipo kuogopa na amini utafanikiwa katika jambo unalotaka kufanya.
JIAMINI NA AMINI UNAWEZA. ISHI NDOTO YAKO.

Post a Comment

 
Top