Kuna juisi za aina mbalimbali na matumizi yake yanategemea na malengo ya mtumiaji. Inawezekana watumiaji wengi wanakunywa juisi bila kujua umuhimu au kazi yake mwilini.
Safu hii itaeleza utumie juisi gani na wakati gani na nitaeleza pia jinsi ya kutengeneza na kazi zake.
JUISI YA TIKITI MAJI
Chukua tikiti maji (Watermelon), osha kisha likate vipande na chukua nyama yake ya ndani ambayo utaisaga na kupata juisi.
Faida yake
Juisi hii ina uwezo wa kusafisha figo pamoja na njia ya mkojo yaani Urethra. Inazuia unene (Obesity) kwa kuwa na kiwango kidogo cha calories.
JUISI YA KAROTI NA APPLE
Hutengenezwa kwa kusaga matunda hayo na kukamua maji yake na maelekezo yake yapo hapo chini.
JINSI YA KUTENGENEZA
Chukua kiasi cha karoti na apple kinachotosha kutengeneza juisi kwa kiasi ulichokusudia. Anza kuandaa juisi yako kwa kuosha na kumenya karoti na apple kisha katakata katika vipande vidogo vinavyoweza kusagika kirahisi kwenye blenda. Saga mchanganyiko wako ili upate juisi.
Baada ya kupata mchanganyiko wa juisi yako unaweza kuongeza asali japokuwa siyo lazima kwa kuwa matunda hayo yana sukari.
Faida yake
Juisi hii ina uwezo wa kutunza ngozi yako kwani tunda la apple linaondoa uchafu kwenye ngozi na karoti nayo kwa kutumia kirutubisho cha beta-karotini chenye uwezo wa kutengeneza vitamini A huweza kulinda na kurejesha uhai katika ngozi ambapo inaifanya ionekane nyororo.
Pia juisi hii huweza kulifanya tumbo lako kuwa safi kwani husafisha tumbo na kuondoa uchafu tumboni. Aidha, juisi hii inafanya ini lifanye kazi yake vizuri kwa kulainisha nyongo na kusaidia kuondoa uchafu.
JUISI YA VIAZI MVIRINGO
Chukua viazi mviringo vinavyotosha kwa juisi. Andaa kwa kuviosha na kumenya kisha katakata vipande vidogo kwa ajili ya kuvisaga. Saga ili upate juisi uliyoikusudia.
Faida yake
Juisi hii inatumika kama dawa ya kuondoa au kupunguza asidi au gesi tumboni. Juisi ya viazi mviringo inaweza kusaidia kupunguza matatizo ya figo, kisukari, unene au kitambi.
JUISI YA MBOGAMBOGA
Juisi hii ina mchanganyiko wa mbogamboga ambazo mtumiaji hupenda kama vile matango, karoti na nyanya. Maandalizi yake ni kama juisi nyingine.
Anza kwa kuosha mbogamboga hizo kisha menya na kukatakata vipande. Saga mchanganyiko huo kwenye blenda ili upate juisi uliyoikusudia.
Faida yake
Juisi hii inasaidia kuzuia kansa hasa ile ya kwenye mfumo wa kumeng`enya chakula, kukinga mapafu na mishipa ya artery. Pia inasaidia kuimarisha kinga.
Kwa aina hizo chache za juisi unaweza kujua umuhimu wa juisi za matunda na mbogamboga tunazotumia. Kwa leo ninaishia hapo, siku zijazo nitaendelea kukupatia ufahamu kwa aina zingine za juisi pamoja na kazi zake
Post a Comment