Jiulize ni ndoto gani uliyonayo unayotaka kuitimiza? Je, una jambo
gani kubwa ambalo unahitaji kulifanikisha kabla ya kuondoka kwako hapa
duniani? Je, una lengo gani kubwa ambalo unahitaji kulitimiza haraka ili
kuleta furaha na amani ndani ya moyo wako? Naamini kila mtu huwa na
ndoto ambayo daima anatamani ifanikiwe katika maisha yake na hatimaye
iweze kuleta furaha ya kweli ndani ya moyo wake. Unahitaji kuifahamu
ndoto yako lakini zaidi kuhakikisha unaifanikisha kwa wakati husika.
Amini unauwezo mkubwa ndani yako na amini hakuna unaloshindwa
kulifanikisha kama ukiamua kufanya hivyo, amini wewe ndie mwenye hatima
yote ya maisha yako na mafanikio yoyote unayoyataka maishani mwako. Kwa
kupitia makala hii nataka ufanye uamuzi wa kutimiza ndoto yako leo hii,
kama unahitaji kufikia kilele cha mafanikio juu ya ndoto yako huu ndio
wakati wa kusoma makala hii ili kujua hatua unazopaswa kufuata na
kuchukua kila siku na hatimaye ndoto yako iweze kuwa kweli na kuleta
uhalisi katika maisha yako.
Hatua tatu muhimu za kukusaidia kufikia ndoto yako.
1: Amini ndoto yako.
Ndio. Jambo la kwanza kabisa unalopaswa kulifanya ili kuhakikisha
unaelekea katika kilele cha utimizaji wa ndoto yako ni kuamua kuiamini
ndoto yako (Believe your dream). Kuamini ndoto yako ni jambo muhimu sana
na la pekee linalohitajika kufanyika na wewe mwenyewe binafsi ndani
yako, kumbuka hakuna mtu anayeweza kuja kwako na kukuaminisha juu ya
kile kitu unachokitaka katika maisha yako wewe ndiye unayepaswa kufanya
hivyo kila siku.
Kuamini ndoto yako maana yake unakubaliana na hicho kitu unachokiona
mbele yako na kujenga picha halisi ndani yako kwamba ipo siku
utafanikiwa na kuifikia ndoto hiyo, haijalishi mazingira gani au
changamoto gani zinakuzuia usifanikiwe. Amini ndoto yako kiasi kwamba
hata kama watu wote wakikaa mbali na wewe na kukuambia jambo hilo
haliwezekani au halitofanikiwa, wewe unaamini litafanikiwa na kuleta
ushindi maishani mwako.
2: Fuata ndoto yako.
Hatua ya pili ni kufuata ndoto yako. Huwezi kubaki unaamini pasipo
kuchukua hatua ya kivitendo kila siku ili uweze kuleta matokeo chanya
kwenye ndoto uliyonayo. Unapaswa kuchukua hatua hata kama ni hatua ndogo
kiasi gani lakini ni muhimu kuweza kufanya hivyo ili kuleta matokeo
makubwa katika maisha yako. Unapoanza kufuata ndoto yako unaanza kuona
fursa na milango mingi zaidi ikifunguka kwa ajili ya kutoa nafasi juu ya
kufanikisha ndoto hiyo.
Mawazo mazuri na watu wa kukusaidia huanza kujitokeza kwa ajili ya
kukupa nguvu na kutembea na wewe katika safari yako ya kuelekea kutimiza
ndoto yako. Hupaswi kukata tamaa haraka juu ya mwendo mrefu ulionao wa
kuifuata ndoto yako bali unahitaji kufanya maamuzi magumu na amua
kujikana hadi uhakikishe unatimiza safari yako uliyoianza. Usikubali
kuishia njiani kisa changamoto au milima unayoipanda ni mingi au hakuna
mtu njiani wa kukupa msaada, kila siku amua kujikana binafsi kuhakikisha
unafika mwisho mwema wa safari yako.
3: Ishi ndoto yako.
Hii ni hatua muhimu unayotakiwa kuipa nafasi kubwa ingawa watu wengi
huwa hawatoi umuhimu juu ya hatua hii. Ni hatua inayoweza kukujengea
heshima, nidhamu na bidii ya kutekeleza majukumu yako ya kila siku
yanayoweza kuwa msaada mkubwa katika kukufikisha kwenye kilele cha
mafanikio ya ndoto yako. Watu wengi huwa wanzani kutambua ndoto zao ndio
mwisho wa kila kitu bali unapaswa kutambua ndoto yako kama unavyojua,
ila jambo kubwa zaidi ni kuishi kwa kuendana na ndoto yako uliyoanayo.
Kuishi kwenye ndoto yako kunakufanya uwe wa pekee na kuleta utofauti
miongoni mwa watu wengi waliokuzunguka, huwezi kuishi kiholela holela na
kujiweka kwenye hali ya kawaida kama umebeba ndoto kubwa ndani yako. Ni
lazima utambue maisha yako yanapaswa wakati wote kuwa kwenye mpangilio
na nidhamu kubwa inayokuonyesha kama mtu mwenye maono na ndoto kubwa
unayokimbilia kuitimiza. Ishi ndoto yako hadi uwe na mwonekano na
taswira inayodhihilishia wengine kile unachokitaka.
Amua kutoa nafasi kila siku kwa ajili ya kutekeleza malengo na
mikakati yako itakayokupa hatua ya juu sana ya kufanikisha ndoto yako,
usikubali kupoteza muda wako wowote kwenye mambo yasiyo na mchango
mkubwa katika ndoto yako bali hakikisha unaweka bidii na msukumo wa
kutosha kila siku katika malengo yako ili uweze kufikia ndoto yako ya
maisha.
Les Brown ambaye ni muhamasishaji wa masuala ya maendeleo ya mtu
binafsi nchini Marekani aliwahi kusema katika moja ya hotuba zake kuwa, “Kama unaweza kuota ndoto basi fahamu unaweza kuitimiza.” Amini
ndoto yako inawezekana, amini unauwezo mkubwa ndani yako wa kufikia
ndoto na malengo yako mazuri uliyonayo. Unachopaswa ni kuamua leo hii
kuishi kulingana na ndoto yako na kuwa na moyo wa dhati kwa ajili ya
kuifanikisha. Amini ndoto yako (believe your dream), Fuata ndoto yako
(follow your dream) na Ishi ndoto yako (Live your dream).
JIAMINI NA AMINI UNAWEZA. ISHI NDOTO YAKO.
Post a Comment