0

Na.Ahmad Mmow, Kilwa.
Mahakama Kuu kanda ya Mtwara jana imetoa uamuzi wa shauri la uchagzi namba 4 la mwaka 2015 kwa kutupilia mbali maombi ya aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM) aliyeomba mahakama hiyo itengue matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi mbunge wa jimbo hilo Vedasto Ngombale (CUF).

Akisoma hukumu ya shauri hilo jaji wa mahakama hiyo, Ignas kitusi alisema baada ya kusikiliza ushahidi uliotolewa na pande zote za shauri hilo na kwakuzingatia sababu zilizoelezwa na mlalamikaji (Mangungu) hazikukidhi vigezo, kwa sababu hoja nyingi zilikosa uthibitisho usiotia shaka.

Hivyo mahakama hiyo ilijiridhisha pasina shaka kwamba matokeo yaliyompa ushindi Veda Ngombale ambae alikuwa anaongozwa na Kutetewa na Mawakili Raynald Songea na Moses Mkapa, dhidi ya Mangungu aliyekuwa anaongozwa na wakili Idd Mtinginjola, ulikuwa huru na haki na haukuwa na kasoro zilizoweza kuathiri matokeo yaliyotangazwana tume ya Uchaguzi katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Alisema katika shauri hilo ambalo mpeleka maombi, Mbungungu aliwalalamikia mwanasheria mkuu wa serikali na msimamizi wa uchaguzi aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, Twalibu Mbasha ambao walitetewa na wakili mwandamizi wa serikali, Salum Mohamed na Pauline Mdendemi. kwamba Mangungu hawakutoa uthibitisho ikiwamo vielelezo ambavyo mahakama hiyo ingeshawishika na kukubalikutengua matokeo.

Badala yake hoja nyingi zilikuwa za hisia nazilikuwa zinaibua maswali mengi yaliyokosa majibu. Kitusi akirejea hukumu mbalimbali za kesi za uchaguzi alisema ili kuthibitisha kulikuwa na ukiukwaji wa kanuni taratibu na sheria kulihitajika ushahidi unaojitosheleza na baadhi ya ushahidi ulihitaji viambatanisho mambo ambayo Mangungu hakutoa wala kuthibitisha.
"Malalamiko hayakueleza msingi wa malalamiko kisheria bali kuna hisia tu, kwa mfano mleta maombi alisema fomu za matokeo hazikuwa na nembo ya tume ya uchaguzi lakini ameshindwa kuthibitisha," alisema jaji Kitusi.

Alibainisha kwamba zipo fursa na hatua zilizowekwa na tume kwa wakala ambae hakuridhika au kuridhika alitakiwa kuzifuata kama ilivyofafanuliwa kwenye sheria ya uchaguzi katika vifungu vya 59 na 60. Ikiwemo matumizi ya fomu namba 21B na fomu namba 16 ambayo inatumika kujaza malalamiko. ambapo matokeo ya rasmi ya ubunge ni yale yanayoonekana kwenye fomu namba 21B.

Hata hivyo mawakala wa mlalamikaji hawakujaza malalamiko, pia hakukuwa na sababu za msingi za kuhesabu tena kura kwenye kituo cha kujumlisha matokeo. Jaji Kitusi alikubaliana na hoja za mawakili wa serikali ambao walisema mtu ambae hakujaza fomu ya malalamiko ushahidi wake hauwezi kutumika, labda pale ambapo zitaelezwa sababu ya msingi jambo ambalo mashahidi wa mlalamikaji hawakufanya.
"Kuhusu ombi la tisa lakutaka mahakama itengue matokeo, natamka kwamba uchaguzi wa ubunge katika jimbo la Kilwa Kaskazini ulikuwa huru na haki na ulifanyika kwa mujibu wa sheria na mlalamikiwa alichaguliwa kisheria, ushindi wake ni halali," alihitimisha jaji Kitusi

Akizungumza baada ya hukumu hiyo Ngombale alisema uamuzi huo unampa nafasi ya kuwatumikia wapiga kura wake. kwamadai kwamba kesi ilikuwa inaathiri utendaji na uwakilishi wake kama alivyowaahidi kwenye kampeni.

Nae Mangungu alisema jaji alishaamua hivyo hakuwa na sababu za kutoa maoni kwani kwakufanya hivyo ni sawa na kumshushia heshima.
"Siwezi kusema kama nitakata rufaa ama sitakata nisingependa pia kuzungumzia hilo ni mapema kulizungumzia," alisema Mangungu.

Katika shauri hilo lililokuwa na mshahidi 26, mangungu alikuwa na hoja 9 ambazo zilisababisha aiombe mahakama itengue matokeo. Hata hivyo hoja zote zilipanguliwa na mawakili wa serikali na wa Ngombale.

Post a Comment

 
Top