0

Mwanasheria wa CHADEMA Tundu Lissu amesema hakuna mtu ndani ya chama ambaye ana lengo la kumjaribu Rais Dkt. Magufuli ikiwa ni siku chache baada ya Rais kutangaza oparesheni UKUTA isifanyike na atakayefanya hivyo atakuwa anamjaribu na yeye hajaribiwi

Lissu ameyasema hayo Jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu barua waliyoandikiwa na Kamishna wa Tume ya Maadili nchini Jaji Salome Kaganda ikiwataka kutoa maelezo kwa nini viongozi wa chama hicho wametoa kauli zenye kuleta uvujifu wa amani nchini.

"Barua tuliyoandikiwa mimi na Mwenyekiti Freeman Mbowe haioneshi kwamba tulitoa kauli hizo wapi lini na saa ngapi jambo ambalo linatia hofu juu ya lengo la mwandishi" Amesema Lissu
Aidha Lissu ameonesha wasiwasi wake kwamba huenda kitendo cha kutumiwa barua hiyo ni maandalizi ya kuvuliwa ubunge yeye na Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe kwa kuwa moja kati ya sababu ambazo zinaweza kumvua ubunge kwa mujibu wa sheria ni kukiuka maadili ya utumishi wa umma.

Lissu ameongeza kuwa CHADEMA itafanya kila kitu kwa kufuata katiba na sheria za nchi na endapo watapata shida katika kutimiza hilo watafuata mkondo wa sheria kwenda mahakamani kudai haki yao.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa chama hicho Vicenti Mashinji amesema UKUTA tayari msingi umeshaanza kuwekwa na itakapofika Septemba Mosi kazi iliyobakia itakuwa ni kuezeka bati nchi nzima.

Post a Comment

 
Top