0

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jana imeshindwa kuendelea kusikiliza kesi ya kukutwa na meno ya tembo yenye thamani ya Sh bilioni 7.4 inayowakabili watu sita wakiwemo maofisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA), kwa kuwa wakili wa utetezi hakuwepo mahakamani.

Kesi hiyo ilitajwa jana kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa lakini Hakimu Mkazi, Huruma Shahidi aliahirisha hadi Julai 26 mwaka huu, kwa kuwa Wakili wa Utetezi, John Mapinduzi hakufika mahakamani.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni maofisa wawili wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambao ni Mohamed Haji (48) na Omary Ally (50), wengine ni kibarua wa Mamlaka ya Bandari Zanzibar, Haider Abdallah (54), Mohamed Mussa, Juma Makame na Mohamed Mashaka.

Wanadaiwa, Novemba 13, mwaka jana katika Bandari ya Zanzibar, walikutwa na vipande 1023 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilogramu 2915 vyenye thamani ya Sh bilioni 7.4 bila kibali.

Katika hatua nyingine, Mahakama imeutaka upande wa Jamhuri katika kesi ya kukutwa na meno ya tembo yenye thamani ya Sh bilioni 5.4 inayomkabili Raia wa ChinaYang Feng Glan na wenzake kukamilisha upelelezi haraka ili kesi isikilizwe.

Hakimu Shahidi alisema hayo jana, baada ya wakili wa mshtakiwa huyo Nehemia Nkoko kulalamika kuwa upelelezi wa kesi hiyo umechukua muda mrefu. Awali, Wakili wa Serikali, Paul Kadushi akisaidiana na Faraja Nchimbi alidai upelelezi wa kesi hiyo, haujakamilika na wanaomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 18 mwaka kwa kutajwa. Mbali na Glan, washtakiwa wengine ambao ni wafanyabiashara raia wa Tanzania ni Salivius Matembo (39) na Manase Philemon (39), washtakiwa wote wanashtakiwa kwa makosa manne.

Washtakiwa wanadaiwa kujihusisha na kuendesha biashara ya nyara za serikali ambazo ni vipande 706 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilogramu 1,889 vyenye thamani ya Sh bilioni 5,435,865,000, mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Post a Comment

 
Top