0

Stop Doing This
Kutimiza ndoto na malengo yoyote yale uliyonayo katika maisha yako, kunahitaji nia ya dhati ya kujitoa na kuweza kuishi maisha yenye misingi inayofuata kanuni na nidhamu mbali mbali zinazoweza kuwa msaada mkubwa wa kukusaidia kufanikisha ndoto yako husika na malengo uliyonayo. Ndio maana kuna wakati unahitaji kuwa na njaa tena njaa kubwa zaidi na shauku iliyokujaa kwa ajili ya kukusaidia kufikia ndoto na maono ya maisha yako.

Unaweza ukawa huelewi hasa ni ninapozunguzia suala la kuwa na njaa ya mafanikio. Kuwa na njaa au shauku ya mafanikio ni jambo muhimu sana kwa mtu yoyote yule mwenye ndoto na malengo makubwa ya kufikia mbali katika maisha yake. Kuwa na njaa ya mafanikio maana yake ni kuwa na shauku iliyopitiliza na yenye kiwango cha juu cha kufikia ndoto yako. Hauwezi kusema unahitaji kufikia ndoto yako hiyo uliyonayo sasa, kwa kubaki unafanya mambo kwa kiwango cha kawaida (level ya chini) au kiwango cha chini kabisa cha kujituma na kujitoa ili kuifikia ndoto husika. Ili ufikie ndoto yako utahitaji kujituma na kujitoa zaidi na zaidi usiku na mchana na zaidi ujenge kiu kubwa ya kuifikia ndoto yako husika pasipo kuchoka.

Na kuna wakati unapokuwa na njaa hiyo ya mafanikio utahitaji kupunguza au kuacha kabisa mambo ambayo hayana nafasi au nguvu ya kukupa hatua yoyote ya kuifata au kuiishi ndoto yako. Mambo hayo unapoyashikilia na kutokuyaondoa katika maisha yako yanaweza yakawa gereza tosha la kukuzuia kuona matumaini na ukweli halisi ya kuifikia ndoto yako. Mambo hayo ni kama ifuatavyo:

1: Punguza au acha kabisa kutumia muda wako vibaya kwa kulala au kuwa usingizini kwa muda mrefu.
Ni vyema ujifunze kuamka asubuhi na mapema na kufanya mambo ambayo yataboresha maisha yako. Amka mapema hata kwa ajili ya kujisomea vitabu, kuandaa vipaumbele vyako vya siku, kufanya mazoezi ya mwili, kufanya maombi na sala, nakadhalika. Donald Trump bilionea na tajiri mkubwa wa kimarekani ambaye kwa sasa anagombea nafasi ya urais kupitia chama cha Republican nchini mwake, ndani ya kitabu chake cha Think like Bilionea anasema huwa analala saa 7 usiku anamka saa 11 alfajiri; na kila anapoamka uanza siku yake kwa kusoma vitabu na magazeti yenye taarifa muhimu za siku hiyo, huku bado ni tajiri na bilionea mkubwa lakini ni ajabu kwa kuona anafanya hivyo tofauti na wengi wetu. Usitegemee mafanikio huku unalala kama mtu aliyepata kila kitu huku ndo Kwanzaa unaanza!!! Kuwa na njaa ya mafanikio na kutimiza ndoto yako uliyonayo (Be hungry).

2: Muda unaotumia vibaya katika mambo yasiyo endana na ndoto yako uliyonayo.
Mambo kama vile kuchati kwa muda mrefu katika mitandao ya kijamii; kuangalia movies; kufanya safari hata zisizo na msingi wowote, nakadhalika. Tena wapo watu wanaotumia muda wao vibaya kwa masuala ya starehe na anasa muda mwingi. Nakuambia huwezi kutoka na kufanikiwa katika maisha kwa kufanya mambo jinsi unayojiamulia tu kila panapokucha; ni lazima ujiwekee utaratibu utakaokuongoza ili kukufikisha katika kilele cha mafanikio yako. Jifunze kufuata moyo wako na si akili. (Follow your heat and not your mind).

3: Chunguza tabia zote zinazokufanya usisogee mbele na kupiga hatua kwenye mafanikio makubwa.
Tabia kama vile za kulalamika; kutokujishusha na kujifunza kwa wengine; wivu na husuda; na nyinginezo ambazo zimekuwa tanzi kwa wengi kufikia mafanikio yao, hata wengine kufikia kuzani wamelogwa kumbe ni tabia zao walizonazo ndio zimefanyika kuwa uchawi wa mafanikio kwenye maisha yao. Acha tabia ya starehe zinazopitiliza hadi kuula uchumi wako; acha kuwa mtu wa kusema wengine waliofanikiwa na kulalamika wakati wote na badala yake jifunze kutoka kwa hao waliofanikiwa badala ya kuwasema kila muda.

4: Uvivu na hali nzima ya kutokujishughulisha kwa kiwango cha juu.
Hakuna mafanikio yanayokuja pasipo kujitoa kwa nia ya dhati kutoka ndani yako. Ni lazima ili ufikie mafanikio makubwa ya ndoto yako huna budi kujituma na kujitoa usiku na mchana kwa kufanya kazi kwa bidii na juhudi ili uweze kupata matunda ya kazi yako uliyonayo. Hasiyefanya kazi hawezi kula au kufanikiwa katika maisha yake; kwa sababu ndoto nyingi zinategemea rasilimali fedha na muda. Unahitaji kutoa muda wako mwingi zaidi katika kujituma na kufanya kazi kwa bidii ili uweze pia kupata fedha itakayokuwa sehemu ya kukupeleka zaidi katika kufanikisha ndoto na malengo makubwa uliyonayo.

5: Punguza au acha kufanya kila kitu na amua kufanya jambo moja (specialize).
Usifanye kila kitu kwani kufanya kila kitu ni kuchagua au kuamua kufeli katika kila kitu. Amua kufanya jambo moja ambalo utalifanya kwa ufanisi hadi ufikie hatua ya kulibobea na hapo ndio utaona matunda ya jambo hilo. Kama ni mjasiriamali amua kujikita zaidi katika ujasiriamali na kujifunza zaidi kila iitwapo leo; kama ni mwandishi kama mimi amua kuwa mwandishi mwenye njaa ya kutimiza ndoto yake nawe utafanikiwa; kama ni muhamasishaji amua kubobea zaidi katika hilo hadi ifikie mahali mji mzima ukutambue kuwa wewe ndie muhamasishaji pekee mjini. Hivyo hivyo kwako wewe msanii, mchoraji, mwimbaji, nakadhalika. Amua kufanya jambo moja na usikimbilie kufanya kila kitu kisa umeona wengine wanafanya; utafeli kufanya namna hiyo.

Maisha yamejawa na kanuni nyingi za mafanikio kama unahitaji kufanikiwa hauna budi kuzifaata kanuni hizo ili uyaone mafanikio hayo yakitokea. Amua kubadilika ili kufikia ndoto yako. Ninakupenda na natamani uone hakika ukweli uliopo pale unapochukua hatua ya kutekeleza mambo haya. Chukua hatua sasa kwa vitendo.
JIAMINI NA AMINI UNAWEZA. ISHI NDOTO YAKO.

Post a Comment

 
Top