0
            PICHA KUTOKA MAKTABA

NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura, jana amekabidhi Bendera ya Taifa kwa kikosi cha timu ya wasichana ya FC Vito Malaika ya Nachingwea, inayokwenda Filnand kushiriki Helisnki Cup 2016.

 Naibu Waziri Wambura alikabidhi barua hiyo jana, katika hafla ya kukiaga kikosi hicho kilicho chini ya umiliki wa Sports Development Aid (SDA) na LiiKe Finland, kinachokwenda kushiriki michuano hiyo inayotarajia kuanza kutimua vumbi Julai 8 hadi 16. 

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Naibu Waziri Wambura aliwataka nyota 12 walio na umri wa miaka 11, kutambua kuwa mamilioni ya Watanzania yako nyuma yao na kwamba wanapaswa kupambana mashindanoni kuhakikisha wanarejea na ubingwa. 

Naye Mratibu wa SDA, Chigogolo Mohamed, aliwataja nyota wanaokwenda mashindanoni kuwa ni Lucy Mwenda, Mwajuma Seleman, Hadija Seifu, Mwajuma Ahamad, Alia Fikiri, Shukuru Mohamed, Maua Mussa na Nasra Badiru. Wengine ni pamoja na Neema Hashimu, Mwanahid Bakari, Sheila Ismail na Kabula Obed, watakaokuwa chini ya Mlezi wao Noela Joseph, kikosi kitakachoongozwa na Kocha Mkuu Bakari Selemani. 

Helsinki Cup, ni michuano ya nne kwa ukubwa miongoni mwa mashindano ya vijana barani Ulaya, ambako mwaka huu yatashirikisha timu zaidi 1,200 kutoka mataifa 15 tofauti duniani na kufanyika kuanzia Julai 8 hadi 16, jijini Helsinki, Finland. Kwa mujibu wa Chigogolo, safari ya FC Vito Malaika Nachingwea kwenda kushiriki Helsinki Cup imedhaminiwa na Niras Ltd, Wärtsilä Tanzania, Amer Sports, Stadium, Abbasi Export Ltd, Orange Technology na Ubalozi wa Finland nchini Tanzania.

Post a Comment

 
Top