Kama unakumbuka hapo awali, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilionekana kujichanganya katika suala la mgogoro wa Stand United.
Lakini sasa inaonekana kuchoshwa na mvutano wa muda mrefu baada ya kuamua kusema inautambua upande mmoja.
Kumekuwepo na mvutano wa muda mrefu katika Klabu ya Stand United kati ya makundi mawili ya Stand United FC na Stand Kampuni.
Awali, TFF ilisimamisha mchakato wa uchaguzi wa klabu hiyo uliopangwa
kufanyika Juni 26, mwaka huu baada ya kupokea barua mbili za uchaguzi
kutoka makundi hayo mawili ambayo kila moja lilikuwa likitaka kufanya
uchaguzi.
Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, amesema: “Katika kikao kilichofanyika
Julai 13, mwaka huu, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imetoa msimamo wake
baada ya kupitia vielelezo vyote na kujadiliana na wadau wa Stand United
na kugundua kwamba jina la Stand United FC ndiyo jina halali
lililosajiliwa na msajili wa klabu na vyama vya michezo hapa Tanzania.
“Uchaguzi uliofanyika hivi karibuni katika Klabu ya Stand United,
umebainika kuwa na sifa zote za kuitwa uchaguzi huru na haki kutokana na
kuwashirikisha wanachama halali wa klabu hiyo.
“Lakini pia TFF inawatambua viongozi waliochaguliwa kwenye uchaguzi huo
na kulitambua daftari la wanachama wa Stand United lililoboreshwa kwa
maelekezo ya TFF.”
Katika hatua nyingine, Kamati ya Rufani ya Uchaguzi ya TFF chini ya
mwenyekiti wake, Mutabaazi Lugaziya, imeitupilia mbali rufani ya mmoja
wa wagombea katika uchaguzi wa Chama cha Soka Mkoa wa Dodoma (Dorefa),
Kuayawaya Kuayawaya kutokana na rufani yake kuonekana haina mashiko.
Kuayawaya alikata rufaa kwenye kamati hiyo akipinga jina lake kukatwa
baada ya kuonekana hana vigezo vya kuwa mgombea katika uchaguzi huo
unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
Post a Comment