0


Dar es Salaam. Waziri Mkuu Mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowasa amemtaka Rais John Magufuli kuwa na utamaduni wa kufanya mazungumzo na wanasiasa wenzake ili kufikia muafaka wa mambo mbali mbali ya kisiasa nchini.

Lowasa ameyasema hayo leo wakati wa mahojiano na Tido Mhando kupitia kipindi cha Funguka kinachorushwa na Televisheni  ya Azam. Lowasa amesema kuwa siasa ni mazungumzo na siyo kutoa tu amri kama anavyofanya Rais Magufuli.

Kadhalika Lowassa amesema kila mtu ana wajibu wa kuheshimu amani ya nchi na hakuna mtu mwenye hati miliki ya nchi hii.

“Serikali haipaswi kuwa na ghadhabu, inapaswa kuwa na tabia ya kuzungumza. Sisi sote ni Watanzania kwa nini tunaogopa kuzungumza. Mazungumzo ndiyo njia bora ya kufikia maridhiano. Pia Rais Magufuli aitazame Zanzibar, tunasikia watu wanashughulikiwa kwa njia mbalimbali, wanakamatwa, hivyo hawezi kuikwepa Zanzibar kwani hilo ni suala lake.” alisema Lowassa.

Pia Waziri Mkuu huyo Mstaafu alisifia kazi nzuri anayofanya Rais Magufuli kama vile kutatua tatizo la madawati nchini na mchakato wa kuhakikisha serikali inahamia Dodoma.

Alisema kuhamia Dodoma ni jambo zuri ila linapaswa kufanywa taratibu na siyo kwenda kwa kasi kama inavyoonekana sasa.

Post a Comment

 
Top