0

 Joseph Mabula Busanji enzi za uhai wake.

MARA: Mungu tuokoe! Kiongozi wa Kanisa la Efatha ambaye pia ni mfanyabiashara wa mpunga, mkazi wa Mtaa wa Nyasura mjini Bunda, mkoani hapa, Joseph Mabula Busanji (picha iliyozungushiwa duara) ameuawa kinyama kwa kuchomwa visu  shingoni na tumboni kisha kuporwa shilingi milioni 2 na mtu asiyejulikana wakati alipokuwa akienda kununua mpunga, Uwazi lina mkasa mzima.
 Waombolezaji wakiaga mwili wa marehemu.

Akisimulia tukio hilo la kikatili lililojiri saa 7 mchana wa Julai 13, mwaka huu, kwenye  Kijiji cha Bitaraguru, mdogo wa marehemu aitwaye Doto Mabula Busanji, alisema mapema saa 4 asubuhi kabla ya tukio hilo, wakiwa nyumbani Mtaa wa Nyasura, mtu mgeni wasiyemfahamu jina wala makazi yake alifika na kuwaambia anauza mpunga nyumbani kwake Mwibagi, Butiama, akamuomba marehemu aende akaununue.

“Kaka aliingia chumbani akatoka na shilingi milioni 2 na magunia matupu ya kuwekea huo mpunga kisha akachukua pikipiki yake yenye namba za usajili T 676 CKB, akampakiza yule mtu, wakaondoka kuelekea Mwibagi.

Kumbe hata hivyo, safari hiyo iliishia njiani Kijiji cha Bitaraguru.
“Ilikuwa saa 8 mchana, mimi nikiwa nimelala kwa mapumziko, alikuja mama mmoja na kuniambia amepata habari kuwa, Jose amechomwa kisu na kuuawa na mtu aliyekuwa ameondoka naye kwenda kumuuzia mpunga.
 “Baada ya kupata taarifa hizo, niliondoka  mimi na mama. Tulipofika Mto Suguti unaotenganisha Kijiji cha Bitaraguru na Mwibagi, tulimkuta kaka amelala chini akiwa amefariki dunia huku damu nyingi zikitiririka tumboni na shingoni kwenye majeraha aliyochomwa kisu,” alisema mdogo mtu huyo.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo,  waliliambia Uwazi kuwa, baada ya marehemu kuondoka na mtu huyo, walipofika Bitaraguru mtuhumiwa huyo alimuomba  marehemu apitie njia ya kichochoroni na walipofika eneo la mto huo bondeni ambapo ni mbali na mji, mtu huyo alichomoa kisu wakati marehemu akiendesha pikipiki na kumchoma kisu tumboni na shingoni na kumsababishia kifo.
Mashuhuda hao walisema kuwa, baada ya ukatili huo, mtu huyo ambaye hajakamatwa, alichukua fedha zote na kutokomea kusikojulikana na kumuacha marehemu akiwa amelala kando ya pikipiki yake.

Marehemu Joseph alikuwa mnunuzi wa mpunga kutoka kwa wakulima kisha kuukoboa na kuuza mchele maeneo ya Nyasura.

Marehemu alizikwa Julai 15, mwaka huu katika Makaburi ya Kijiji cha Tamau, Bunda ambapo ibada ya mazishi iliongozwa na Mchungaji wa Kanisa la Efatha, Shadrack Mkunda wa Tarime. Kanisa hilo ni tawi la Kanisa la Efatha lenye Makao Makuu jijini Dar chini ya Nabii Josephat Mwingira.

Polisi wilayani Bunda wamethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kwamba wanaendesha msako mkali ili kumtia mbaroni muuaji huyo.

Post a Comment

 
Top