WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewahakikishia Watanzania kwamba Serikali inaendelea na jitihada za kuondoa tatizo la uhaba wa sukari nchini ambapo jumla ya tani 20,000 zilisambazwa jana katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema shehena nyingine ya tani 35,000 inatarajiwa kusambazwa hivi karibuni katika kanda zote nchini hivyo amewataka wafanyabiashara watakapoipokea kuiuza kwa wananchi bila ya kuificha na bei isizidi shilingi 2,200.
Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo jana jioni ( Ijumaa, Juni 10, 2016) wakati akizungumza na Masheikh na Viongozi wa Kamati ya Amani ya mkoa wa Dar es Salaam alipowaalika katika futari aliyoiandaa nyumbani kwake.
Amesema tayari viwanda vimeanza kufunguliwa na tani 300 zilizotoka katika kiwanda cha Sukari cha Kagera zitasambazwa katika wilaya za Kakonko, Kibondo, Kasulu, Uvinza na Kigoma ili kutosheleza maeneo hayo.
Hata hivyo amewataka Maofisa Biashara katika Halmashauri zote nchini kuendelea kufanya ufuatiliaji katika maduka ili kuhakikisha bidhaa hiyo inapatikana na hakuna mfanyabiashara atakayeificha.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu aliwataka wafanyabiashara kote nchini kutopandisha bei za vyakula katika kipindi cha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Akizungumza kuhusu tabia za baadhi ya wafanyabiashara wanaopandisha bei za bidhaa hasa vyakula katika kipindi hiki cha mfungo amewataka kumuogopa Mwenyezi Mungu kwa sababu kitendo hicho kinawapa wafungaji wakati mgumu.
“Kufunga Ramadhani si jambo la anasa, si matashi binafsi bali ni jambo la kiimani hivyo tusipandishe bei ya bidhaa kwa lengo la kuwaadhibu Waislam kwa sababu tu wamefunga.
“Katika Quran surat Baqarah aya ya 183 inasema kwamba enyi mlioamin imefaradhishwa kwenu kufunga kama walivyoamrishwa kufunga kwa waliopita kabla yenu ili muwe wachamungu, hivyo hatuna budi kufunga” alisisitiza.
Alisema tabia hiyo si nzuri na imekuwa ikijitokeza mara kwa mara unapofika wakati wa mfungo kwa wafanyabiashara kuamua kupandisha bei hivyo aliwataka waiache kwani Serikali haitawavumilia na atakayethubutu hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Post a Comment