0

DAR ES SALAAM: Katika kudhibiti biashara ya usafirishaji wa madawa ya kulevya nchini,  Marekani imeleta mbwa wenye uwezo wa hali ya juu katika kutambua madawa ya kulevya na nyara za serikali, ambao wamewekwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam na viwanja vingine.

Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege nchini, ACP Martin Otieno aliliambia Risasi Mchanganyiko kuwa ukaguzi wa mizigo ya wasafiri, bila kujali hadhi yao, hufanywa katika maeneo yote yanayopitisha mizigo, kwa abiria wa kawaida na hata VIP.

“Hakuna exceptional (maalum), kila mtu anakaguliwa, tuna mashine maalum pamoja na mbwa ambao tumepewa na Marekani, wana uwezo wa kutambua aina zote za madawa na nyara, wanakagua mizigo yote na watu wote hata wale wanaopita mlango wa watu mashuhuri (VIP), wote wanakaguliwa,” alisema.

Kamanda Otieno alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa kuhusu madai ya watu mashuhuri kutumika kusafirisha madawa hayo yanayopigwa vita dunia nzima, kwa maelezo kuwa wao na mizigo yao, haikaguliwi kwa sababu ya heshima na vyeo vyao.

“Hakuna mtu anapita hapa bila kukaguliwa, hata viongozi, wao na mizigo yao yote lazima ikaguliwe, iwe ni Waziri, Mbunge au kiongozi yeyote, mfanyabiashara mkubwa, kila mtu hapa lazima apite kwenye mashine yeye na mizigo yake,” alisema Otieno.

Kumekuwa na madai ya muda mrefu kuwa watu maarufu, hasa wasanii wamekuwa wakitumika kusafirisha madawa hayo kwa kinachodaiwa kuwa wao hawakaguliwi.

Miaka michache iliyopita, Video Queen Agnes Gerald ‘Masogange’ alikamatwa uwanja wa ndege jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini akiwa na aina mojawapo ya madawa ya kulevya akitokea Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere ambako inadhaniwa alipita bila kukaguliwa.

Post a Comment

 
Top