Ndugu Wananchi, Nawashukuru sana kwa kujitokeza kwenu kuitikia wito wetu wa kuja kutusikiliza. Tumewaita hapa ili kuwaeleza kinachoendelea katika nchi yetu hivi sasa na madhara makubwa yanayoweza kutokea iwapo hatutosimama kidete dhidi ya mbinu zozote za kufifiza na kuminya demokrasia na misingi ya uwajibikaji katika nchi yetu.
Mwaka 2015 tulikwenda kwenye uchaguzi kuchagua madiwani, wabunge na Rais. Baada ya Uchaguzi kumalizika Serikali mpya iliundwa na Serikali za Mitaa (Halmashauri) kuundwa. Nawapongeza wananchi wote kwa kuendesha zoezi la uchaguzi kwa amani na kuweka heshima ya nchi yetu mbele.
Baada ya uchaguzi tumeona viongozi wapya wakichukua hatua mbalimbali nzuri na mbaya, zenye kujenga na kubomoa, zenye kuimarisha demokrasia na zinazobomoa demokrasia. Tumeshuhudia maamuzi mengine ambayo yanatia khofu, kwamba ingawa tunaona dhamira ya dhati ya kupambana na Ufisadi, lakini pia tunaona mbinu za chini chini za kutokomeza Demokrasia ya nchi yetu ambayo tumeijenga kwa jasho na damu.
Mkutano wetu wa leo utagusia baadhi ya maeneo ambayo tunadhani ni vihatarishi vya ustawi wa wananchi wetu na ambavyo lazima tuanze kuvipinga mapema sana kabla havijaota mizizi. Ndugu Wananchi, Baadhi ya maeneo tutakayozungumza leo ni pamoja na;
Wabunge kusimamishwa kazi za Bunge
Maamuzi ya Serikali kuhusu Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma
Hali ya Zanzibar
Mwelekeo wa Bajeti ya Kwanza ya Serikali ya Rais Magufuli
Tishio la Nchi kuelekea kwenye Utawala wa Imla wa MTU mmoja
Wabunge Kusimamishwa Kazi.
Ndugu Wananchi, mnamo tarehe 30 Mei, 2016 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Naibu Spika lilipitisha Azimio la Bunge la kuwasimamisha kazi wabunge 7 kwa vipindi mbalimbali. Wabunge wawili, ndugu Esther Bulaya na ndugu Tundu Lissu walisimamishwa Mikutano miwili ya Bunge. Wabunge Wanne, ndugu Halima Mdee, Ndugu Pauline Gekul, Ndugu Godbless Lema na Mimi ninayezungumza nanyi tulisimamishwa mkutano mmoja, huu unaoendelea wa Bajeti, na mbunge mmoja ndg John Heche Suguta amesimamishwa vikao 10 vya mkutano huu wa tatu unaoendelea.
Sababu iliyoelezwa na Bunge ni kwamba wabunge hawa walifanya fujo siku ya tarehe 27 Januari, 2016 kufuatia hoja niliyoitoa Bungeni ya kutaka mjadala kuhusu sababu za hovyo na za uongo zilizotolewa na Serikali kuhusu uamuzi wa kuzuia Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) pamoja na televisheni binafsi (Star tv na Azam) kuonyesha moja kwa moja mikutano ya Bunge.
Ndugu Wananchi, mimi binafsi pamoja na wabunge wengine 6 hatukufanya fujo yeyote ndani ya Bunge. Kosa letu kubwa ni kutaka kuhoji maamuzi ya Serikali ambayo kwa maoni yetu hayana msingi wowote. Serikali inasema ninyi Wananchi hamfanyi kazi kwa sababu Bunge linaonyeshwa wakati wa kazi. Hata hivyo Serikali hiyo hiyo inatwambia kuwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita uchumi wa Tanzania ulikua kutoka tshs 16 trilioni mwaka 2005 mpaka tshs 99 trilioni mwaka 2015. Kipindi chote hiki Bunge lilikuwa linaonyeshwa moja kwa moja na televisheni ya Taifa (TBC) na televisheni ya StarTV.
Kama mngekuwa hamfanyi kazi Uchumi usingekua kwa kiwango hicho cha asilimia 600 ndani ya Muongo mmoja wa uongozi wa Rais Jakaya Kikwete. Utawala wa Rais John Magufuli unataka kutuaminisha kuwa ukiwa na Bunge ‘live’ watu hawafanyi kazi lakini uongozi uliopita umedhihirisha kwa ushahidi kuwa ukipanua demokrasia na kuwaonyesha wananchi kila kinachoendelea Bungeni uwezo wa kazi unaongezeka na uwezo wa wananchi kuwajibisha viongozi wao unaongezeka.
Hivyo Serikali kuamua kuficha Bunge ni mbinu za kuendesha Serikali kwenye giza ili kufanya maamuzi ambayo baadaye ionekane Serikali tu au Rais tu ndiye mfanya kazi. Ndio maana mikutano yote ya Rais anapohutubia huonyeshwa moja kwa moja lakini sio Bunge.
Wananchi, Wabunge wamesimamishwa kwa sababu ya kukataa Bunge kuendeshwa kwenye giza. Wabunge waliosimamishwa walisimama kidete kuhoji sababu za Serikali kufikia maamuzi hayo. Walitaka kujua kwanini Serikali imekuwa kigeugeu kwa kubadilisha badilisha sababu zake za kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya Bunge.
Wakati mmoja Serikali ilisema sababu ni gharama, kama ni hivyo ni kwanini walizuia StarTV na AzamTV kuonyesha moja kwa moja? Ni dhahiri wananchi Serikali inataka kuendesha mambo yake kwa uficho kwa sababu kuna maamuzi inataka kufanya na haitaki wananchi mjue mapema maamuzi hayo. Serikali inaturudisha nyuma badala ya kwenda mbele.
Wananchi, wabunge waliosimamishwa ni wabunge wenye uwezo wa kujenga hoja. Kuna wengine wamebaki Bungeni wenye uwezo mkubwa tu wa kujenga hoja, lakini hawa saba waliosimamishwa ni wabunge waliojidhihirisha kwa muda mfupi kwa baadhi yao kama ndugu Heche, kwamba wanaweza kusimamia hoja zao bila woga. Swali la kujiuliza ni, tukio ambalo limetokea mwezi Januari ni kwanini lifanyiwe mwezi Juni tena wiki moja tu kabla ya Waziri wa Fedha kuwasilisha Bungeni Bajeti ya Serikali?
Katika waliosimamishwa ni pamoja na Waziri Kivuli wa Fedha, ndg. Halima Mdee na Waziri Kivuli wa zamani wa Fedha ambaye anazungumza nanyi leo (Zitto Kabwe). Kuna nini? Nitawaeleza katika hoja ya Bajeti. Kimsingi Utawala wa Rais Magufuli umepanga kupandisha kodi za wananchi masikini na uliona uwepo wetu bungeni utatibua mipango yao.
Rais na wenzake ndani ya CCM hawapendi kusikia hoja zinazowapinga, hawana uvumilivu wa kukosolewa na hivyo walipanga kuhakikisha kuwa baadhi yetu hatutakuwepo kwenye mjadala wa Bajeti ili kufanikisha malengo yao ya kufanya maamuzi yatakayowandamiza wananchi.
Nitaeleza vizuri hili baada ya muda kidogo. Hivyo nataka Watanzania wajue kuwa kusimamishwa kwetu ni ajenda maalumu ya Serikali ya Rais Magufuli kufunika mjadala wa Bajeti kwa sababu inajua kuwa tunajua inachopanga kufanya dhidi ya mafukara wa nchi yetu.
Sisi hatutakaa kimya, tutatumia wenzetu waliopo Bungeni kuyasema haya na pia tutazungumza na wananchi kuwaeleza pia.
Tutatumia mikutano yetu mbalimbali bila kujali itikadi za vyama vyetu kuhakikisha kuwa Wananchi wanajua kila kinachoendelea na kuwataka kuunganisha nguvu kukataa udikteta unaonyemelea nchi yetu.
Wanafunzi 7800 Kufukuzwa Chuo Kikuu Cha Dodoma.
Ndugu Wananchi, mmesikia sakata la Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma waliokuwa wanasomea programu maalumu ya Ualimu wa Sayansi. Hawa ni watoto wa Watanzania masikini waliokubali kuacha kwenda Kidato cha Tano na cha Sita (A level) na kukubali kusomea diploma ya Ualimu ili wakawafundishe watoto wa masikini wenzao. Wanafunzi hawa hawakuanzisha wao program hii, ilianzishwa na Serikali na kupitishwa na Baraza la Mawaziri ambalo Rais Magufuli alikuwa mjumbe na alishiriki kikao hicho kwa mujibu wa kumbukumbu za Baraza la Mawaziri.
Rais Magufuli hakupinga mpango huu na aliubariki kama Wenzake walivyofanya na kuanza kutekelezwa. Lengo na program hii ni kuondoa tatizo la walimu wa masomo ya Sayansi. Tanzania ina uhaba wa walimu wa Sayansi 26,000 (Kwa Utafiti wa Mwaka 2014) na tukienda kwa utaratibu wa kawaida tutahitaji miaka 20 kuziba pengo hilo.
Program hii ilianzishwa ili kuziba pengo hili kwa muda mfupi, na vijana waliitikia wito huu wa kizalendo kuhakikisha wadogo zao hawakosi walimu siku za usoni. Serikali ya awamu ya Tano imewafukuza vijana hawa 7800 kutoka chuoni ndani ya masaa 24 kwa makosa ambayo sio yao.
Wananchi, hatusemi kuwa program haikuwa na kosoro. Zilikuwepo ikiwemo kudahili wanafunzi wengi zaidi ya ilivyotarajiwa na kudahili wanafunzi 88 kati ya 7800 ambao walikuwa na daraja la nne (Div 4) katika masomo yao. Lakini aliyedahili sio watoto hawa bali ni Serikali yenyewe, kwanini waadhibiwe watoto?
Bunge lilipotaka kujadili hoja hii au hata kuipeleka kwenye kamati ya Bunge kuifanyia uchunguzi na kutoa mapendekezo Naibu Spika alizuia hoja ya mbunge Joshua Nasari bila sababu za msingi. Wabunge wote bila kujali vyama vyao walitaka hoja ijadiliwe na kuweza kupata majawabu. Mbona wakati wa Uongozi wa awamu ya 4 tulijadili hoja ya mgomo wa madaktari na kisha kupelekwa kwenye kamati ya husika ya bunge kupata suluhisho la kudumu? Kwanini Utawala wa Rais Magufuli hautaki Bunge lifanye kazi yake? Mbona yeye Rais kaenda kujadili jambo hilo huko Chuo Kikuu mlimani?
Wananchi, Rais Magufuli anafikia kuita watoto wetu Vilaza? Rais huyu anayesema yeye ni Rais wa masikini anaita watoto wa masikini Vilaza. Vijana hawa Wazalendo waliojitoa muhanga kuacha kwenda kidato cha Tano ili wasome kuwa Walimu na kulea kizazi kijacho Rais wao anawaita vilaza. Rais sifa zimempanda kichwani. Rais Magufuli hana budi kuwaomba radhi vijana hawa na wazazi wao.
Kitaaluma Rais ni Mwalimu, anajua madhara ya kisaikolojia kufuatia maneno aliyoyasema. Ni sawa na Jenerali wa Jeshi anayetukana askari wake walio Mstari wa mbele. Hata Baba wa Taifa hakuthubutu kamwe kuita wanafunzi Vilaza hata kama walimuudhi kiasi gani.
Rais Magufuli anaongea mno, sio sawa kwa Kiongozi. Rais ajue kuweka akiba ya maneno. Yeye ni Kiongozi wa wote, wenye akili na Vilaza. Yeye anapaswa kuwa wa mwisho kuongea ili watu waweze Kukata rufaa kwake. Yeye akishaongea wananchi ‘aggrieved’ (walioonewa Au kukosewa) waende kwa nani? Waende kwa mungu?
Tunamtaka Rais awarudishe wanafunzi Hawa Chuoni mara moja na wale wanafunzi ambao itaonekana hawakuingia kwenye programu kihalali (ambao Ni 88 Tu) waondolewe badala ya kuadhibu watoto wote kwa makosa ya wachache ambao ni asilimia 5 tu ya wote.
Makosa madogo ni mambo ya kawaida katika Jamii. Yeye Rais ni mfano mzuri wa hili kwani naye mbona aliteua Waziri mlevi na kurekebisha kwa kumfukuza peke yake?, mbona hakufukuza Baraza zima la mawaziri kwa ulevi wa Waziri mmoja?
Zanzibar.
Ndugu Wananchi mnajua mara baada ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar kufutwa chama chetu kiliweka msimamo wa wazi kwamba kinatambua ushindi wa Maalim Seif Sharif Hamad kama Rais aliyechaguliwa na Wazanzibari na anayepaswa kula kiapo na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Tuliandika pia masuala 10 muhimu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuyafanyia kazi, na moja ya jambo tulilomtaka Rais Magufuli Kulifanyia kazi ni suala la demokrasia ya Zanzibar.
Rais hakusikia wito wetu na aliruhusu ufutwaji usio halali, kisiasa wala kisheria wa uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 25, 2015.
Tunarudia kusisitiza kuwa Chama chetu cha ACT Wazalendo hakiutambui uchaguzi wa marudio wa Zanzibar uliofanyika mwezi Machi mwaka 2016 pamoja na matokeo yake yote. Kwa maana hiyo hatutambui Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Baraza la Mawaziri la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na Pia Rais wa Zanzibar.
Wananchi, Hivi karibuni kumekuwa na kuongezeka kwa sintofahamu huko Zanzibar kufuatia Mgombea Urais aliyeshinda na kunyanganywa ushindi wake kwenda kwa wananchi kuzungumza nao.
Hali hii imepelekea jeshi la polisi kumhoji Maalim Seif na siku mbili baadaye Dkt. Shein kutamka kuwa hamwogopi Maalim Seif kwa sababu “Hana vifaru na mizinga”.
Tunalaani kauli hii ya Dkt. Shein ya kutisha kwa vifaru na mizinga. Kamwe huwezi kuzima haki za Wananchi kwa vifaru na mizinga. Dkt Shein akumbuke kuwa Sultan alikuwa na jeshi, vifaru na mizinga na ulinzi wa Dola kubwa kama Uingereza lakini aliangushwa na wananchi wa Zanzibar mwaka 1964.
Dkt Shein akumbuke kuwa nchi kadhaa duniani zilikuwa na madikteta wenye vifaru na mizinga lakini waliondoka. Dkt Shein afute kauli yake hii na kuacha vitisho badala yake aanze mchakato wa kupata maridhiano ya jamii ya Zanzibar. Hatutaki kurithi damu, tunataka kurithi nchi yenye amani, haki na demokrasia.
Wananchi, sisi ACT Wazalendo, tunajua hali mbaya ya kisiasa iliyopo Zanzibar na mkwamo uliopo hivi sasa Kisiasa, Kijamii na Kiuchumi. Hata hivyo ni lazima tupate jawabu kupitia sanduku la kura.
Tunapendekeza kuwa Vyama vikuu vya siasa Zanzibar vikubali ‘kufa kidogo’ yaani ‘to die a little’, kwa vyote kukubali kuwa Chaguzi zote Mbili, wa Mwaka 2015 na ule wa mwaka 2016 zilikuwa batili, zifutwe na Uchaguzi Mkuu mpya uitishwe.
Uchaguzi huo utanguliwe na Serikali ya Mpito itakayohusisha vyama vyote vya siasa na baadhi ya wanajamii wanaoheshimika na Wazanzibari wote ili kujenga kuaminiana.
Tunadhani hii itatupa nusra kwa Zanzibar. Tunawaomba Wazanzibari watumie mwezi mtukufu wa Ramadhani kutafakari maoni haya na wote kwa pamoja baada ya Ramadhani kuja na jawabu ya hali ya kisiasa. Tunatamani Zanzibari irudi kwenye hali ya kawaida na ishamiri.
Zanzibar ikiingia kwenye mtafuruku Tanzania nzima itakuwa kwenye mtafaruku. Ni dhahiri kuwa Rais Magufuli ameshindwa kutoa uongozi kwenye suala hili na hivyo ni wajibu wa Wazanzibari wenyewe kukaa na kupata mwafaka wa kijamii na kusonga mbele.
Bajeti ya 2016/17.
Wananchi, kuanzia tarehe 8 mwezi Juni, 2016 Bunge litakuwa kwenye mjadala wa Bajeti ya kwanza ya Serikali ya Rais Magufuli. Rais ameleta mapendekezo ya Bajeti ya shilingi 29.5 trilioni. Katika makadirio haya vyanzo vya ndani ni shilingi 18.5 trilioni na misaada ni shilingi 3.6 trilioni. Serikali inatarajiwa kukopa jumla ya shilingi 7.4 trilioni.
Mwaka 2015/16 Serikali ilitarajiwa kukusanya jumla ya shilingi 13.8 trilioni, hivyo ndani ya mwaka mmoja wa fedha Utawala wa Rais Magufuli unataka kukusanya shilingi 4.7 trilioni zaidi sawa na ongezeko la asilimia 25. Kwa ufupi ni kwamba Serikali haina budi kuongeza kodi kwa kiwango cha asilimia 25 ili kuweza kutimiza malengo yake ya makusanyo.
Wananchi, mtakumbuka kuwa mara baada ya Rais Magufuli kuingia madarakani tulikuwa tunaelezwa kodi iliyokusanywa kila mwezi na tuliona wafanyabiashara wakikabwa koo kwa kukwepa kodi. Hata hivyo ongezeko la Makusanyo lilikuwa kwa miezi 2 tu ya Novemba na Disemba kwani kuanzia mwezi Janauri makusanyo yalianza kuendana na hali halisi ya uchumi wa nchi yetu na ndio maana mbwembwe za makusanyo hazisikiki tena hapa nchini.
Ukweli ni kwamba Rais alikuwa anakusanya ‘arrears’ na hapakuwa na hapajakuwa na mbinu mpya za kukusanya mapato ya Serikali. Maeneo muhimu yanayopoteza mapato kama vile makampuni ya nje kutumia mbinu za kihasibu kukwepa kodi hayajatazamwa kabisa na Rais na wasaidizi wake.
Hivyo, Serikali imeamua kurudi kwa wanyonge kuwaminya na kodi ikianzia kuchukua kodi zote za Majengo kutoka kwenye Halmashauri zetu. Kodi za majengo ndio chanzo kikuu cha mapato ya Halmashauri zetu za Miji, Manispaa na Majiji. Uamuzi wa Serikali kuchukua chanzo hiki cha mapato utapelekea Halmashauri zetu kushindwa kuzoa taka na hata kutoa huduma kwa wananchi.
Hata hivyo wananchi uamuzi huu ni kwa sababu Halmashauri nyingi za Miji zinaongozwa na vyama vya Upinzani kama vile Manispaa ya Kigoma Ujiji, Manispaa ya Iringa, Arusha jiji, Ilala, Kinondoni, Mbeya Jiji nk. Utawala wa Rais Magufuli unataka kuhakikisha kuwa Manispaa zinaoongozwa na vyama vya upinzani zinashindwa kutoa huduma. Duniani kote kodi za majengo hukusanywa na Serikali za Mitaa. Katika Bajeti ya mwaka huu kodi hizi zitaongezwa maradufu.
Wananchi, Serikali inatarajia kupandisha ushuru kwenye soda, vilevi na sigara pia kwa mujibu wa vitabu vya Bajeti vilivyogawiwa kwa wabunge. Hata kodi kwenye gharama za kupiga simu zitaongezwa kwa zaidi ya asilimia 10. Eneo la ushuru peke yake Serikali inataka kukusanya shilingi 1.2 trilioni kutoka shilingi bilioni 900 za mwaka uliopita. Hii ni nyongeza ya shilingi 300 bilioni zaidi kutoka Bajeti ya mwaka 2015/16.
Maeneo haya mawili peke yake (kodi za majengo na ushuru wa bidhaa) yataongezewa kodi kiwango cha kuumiza sana wananchi wa kawaida. Hii ndio sababu Serikali imefukuza baadhi ya wabunge mahiri bungeni ili kulainisha upitishwaji wao wa viwango hivi vya kodi. Hata hivyo tutatumia wabunge waliobakia Bungeni kuhakikisha kuwa kodi kwa wananchi masikini haziongezwi kiholela.
Wananchi, sisi tunaamini kuwa Bajeti ya shilingi 29.5 trilioni ya Utawala wa Magufuli sio bajeti halisi kwani makadirio yao hayazingatii ukuaji wa uchumi na yana lengo la kuchukua fedha kutoka kwa wananchi kupeleka Serikali jambo ambalo litadidimiza uchumi wa nchi yetu.
Tishio la Demokrasia.
Wananchi jambo la mwisho ambalo ninataka kuwaeleza ni tishio lililopo mbele yetu dhidi ya demokrasia ya vyama vingi. Hatua mbalimbali ambazo Utawala wa Rais Magufuli unachukua ni ishara ya kutengeneza utawala wa Kiimla. Rais ndiye anayejua kila kitu na ndiye anayeamua kila kitu. Hii ni hatari sana kwa nchi yetu na ni lazima kuchukua hatua mahususi kumkatalia Rais mwanzoni kabisa ili asizoee.
Tunarudia kuwa tulimuunga mkono Rais toka mwanzo katika vita dhidi ya Ufisadi, kwani ni vita muhimu na lazima ipiganwe bila kujali itikadi za vyama. Hakuna namna unaweza kumlaumu Rais anapochukua hatua za kusafisha Uvundo katika nchi. Tutaendelea kumwunga mkono katika eneo hilo.
Wananchi, hata hivyo Rais anatia Khofu mno katika ujenzi wa mfumo wa uwajibikaji. Tanzania ina vyombo vya kuimarisha uwajibikaji, ikiwemo Bunge la Jamhuri ya Muungano na Pia Ofisi ya Ukaguzi ya Taifa. Rais anataka kupigana dhidi ya ufisadi nje ya mfumo jambo ambalo ni la hatari sana kwa nchi kwani akitoka yeye tutaanza upya.
Inawezekanaje Kiongozi anayepambana na rushwa akavunja nguvu ofisi ya ukaguzi ya Taifa kwa kumnyima Bajeti Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG)? Rais amediriki hata kuvunja Katiba na sheria ya ukaguzi, kwani Bajeti ya CAG haipangwi na Serikali bali hupangwa na Kamati ya Bunge. Rais ameenda kinyume na sheria na badala yake kapanga mwenyewe Bajeti ya CAG? Toka lini mkaguliwa akapanga bajeti ya anayemkagua? Kamati ya Bunge ilipanga Bajeti ya tshs 69 bilioni kwa CAG lakini Serikali (mkaguliwa) imeipiga panga mpaka tshs 32 bilioni. Hii ni moja ya mfano dhahiri kabisa wa Serikali kuanza kuvunjavunja vyombo vya uwajibikaji.
Wananchi, hivi sasa kuna Ukosefu wa Sukari nchini. Rais alisimama kwenye Vilinge vya Siasa, akatoa matamko makali kwamba kuna Wafanyabiasha wameficha sukari na tukaonyeshwa sukari hiyo. Hata hivyo baada ya siku chache vyombo kama PCCB na TRA vikasema sukari ile ni halali. Inakuwaje Rais alitamka maneno yale bila ya kushauriana na vyombo? Ni dhahiri Rais anaongea na kuropoka tu na kutaka kujenga utawala wa Kimla. Leo bado kuna shida ya sukari na sukari ambayo serikali inasema iliagiza haionekani. Ipo wapi?
Wananchi, Rais Huyu Huyu alikwenda Benki Kuu na kusema nusu ya wafanyakazi pale ni hewa. Mpaka leo hatujaona hao wafanyakazi hewa wa BoT. Rais alikwenda tu kwa kupata maneno ya kuokoteza barabarani na kutoa matamko ambayo yanashusha hadhi ya Benki, lakini Rais anashindwa kutoka mbele kusema alikosea. Tunajenga mfumo mbaya sana wa uongozi wa Nchi.
Leo tunataka kumwambia Rais kuwa aongoze, asitawale. Rais awe na Utu na wananchi wake. Rais awe anasikiliza kwanza na kuchambua mambo kabla ya kusema chochote mbele ya hadhara. Rais awe wa mwisho kusema ili kama kuna rufaa Watu waseme kwake. Vinginevyo Rais anataka kujenga utawala wa Kiimla, tutamkatalia wazi wazi.
Wananchi, nimalizie kwa kusema yafuatayo. Rais John Magufuli amesema kuwa yeye amejitoa muhanga kupambana na ufisadi. Sisi tunalazimika kujitoa muhanga Kulinda Demokrasia.
Ni imani yetu kuwa Ufisadi utapigwa vita kikamilifu sio kwa kutegemea nia ya mtu mmoja bali kwa kuboresha na kutumia misingi ya demokrasia kwa kujenga taasisi madhubuti zitakazomaliza janga la ufisadi bila ya kutegemea nia ya Rais.
Sisi tunaamini kuwa ni jukumu letu kusimama kujitoa mhanga kuzuia maafa ya kitaifa yatakayoweza kutokea kutokana na makosa ya kukandamiza demokrasia na uhuru wa mawazo kwa kuhoji, kukosoa na kurekebisha makosa hayo sasa bila kuchelewa.
Tunamwunga mkono Rais kutokomeza Ufisadi lakini TUNAMPINGA Rais Kutokomeza Demokrasia. Demokrasia yenye misingi madhubuti ya Uwajibikaji ndio jawabu sahihi dhidi ya ufisadi na unyonyaji nchini kwetu.
Nawashukuru sana.
Zitto Ruyagwa Kabwe
Dar es Salaam
Juni 5, 2016
Post a Comment