KATIBU wa Bunge, Dk Thomas Kashillilah
leo ataeleza kinachoendelea kuhusu kusudio la Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni kutaka kumwondoa madarakani Naibu Spika, Dk Tulia Ackson
Kambi
hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) Taifa, Freeman Mbowe katika migomo yake dhidi ya vikao
vinavyoongozwa na Dk Ackson, iliwasilisha kusudio hilo kwa Ofisi ya
Spika wa Bunge wiki iliyopita kwa maelezo kuwa haina imani naye.
Kwa mujibu wa Dk Kashillilah, ataeleza
kinachoendelea leo baada ya kumaliza kupitia taratibu zote na
kujiridhisha kuhusu kila hatua inayopaswa kufuatwa kuhusu suala la aina
hiyo. “Nitaeleza kinachoendelea kesho (leo) baada ya kujiridhisha kuhusu
taratibu zinazopaswa kufuatwa kuhusu suala hilo,” alisema.
Katika kusudio hilo lililowasilishwa na
Mbunge wa Simanjiro, James ole Millya, Kambi hiyo ya Upinzani ilieleza
mambo sita yaliyoisukuma kuona kuwa Dk Tulia hafai kuendelea kushika
kiti cha Naibu Spika.
Mambo hayo ni upendeleo kwa wabunge wa
CCM, kusimamia maslahi ya Serikali badala ya umma, kutokuwa mwanasiasa,
jambo linalomfanya akose uzoefu wa kuendesha vikao vya Bunge, ubabe,
unyanyasaji kwa wabunge wa upinzani na kusimamia fedha za Mfuko wa Bunge
zirudishwe kwa Rais.
Millya alisema walipeleka kusudio hilo
kwa Ofisi ya Spika kwa kuzingatia ibara ya 85(4) ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inayozungumzia hatua za kuchukua ili kumwondoa
madarakani Naibu Spika.
Post a Comment