Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye .
Siku hiyo ambayo hutumika kushinikiza mataifa kutengeneza sheria rafiki za vyombo vya habari zinazoweza kuhakikisha uhuru wa habari katika nchi zao, kitaifa nchini inafanyika mkoani Mwanza leo na kesho.
Mgeni rasmi atakuwa Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (Misa), Simon Berege alisema jana kuwa maadhimisho hayo ni njia pekee ya kujadili na kukumbuka gharama ambayo watu binafsi wanalipa kwa kutoa habari.
“Hii ni siku ya kuwakumbuka waandishi wa habari, kwa namna ya pekee wakati mwingine kwa kutoa kwao habari wanahatarisha maisha yao na kuweka hatarini uhuru wao wenyewe ili sisi tuweze kupata habari vizuri na kuufahamu ukweli,” alisema Berege.
Ofisa Mipango Mfuko wa Vyombo vya Habari (TMF), Raziah Mwawangu alisema waandishi wa habari wamechangia maendeleo ya Taifa kwa kiasi kikubwa.
Katibu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena alisema bado kuna changamoto zinazohitaji umakini kuzipatia ufumbuzi.
“Licha ya Rais kusifiwa kwa hatua mbalimbali anazozichukua dhidi ya matukio fulani, lakini Serikali yake imelifuta gazeti, hatujui kwa kipindi cha miaka mitano tutakuwa wapi, hatujui mweleko thabiti wa Serikali hii,” alisema na kuongeza.
‘‘Jambo lingine ambalo bado linahitaji busara ni hili la Bunge kusitisha matangazo yake ya moja kwa moja badala yake tunaonyeshwa vitu ambavyo vimesharatibiwa, uhuru wa habari hapa uko wapi? Tunaomba wadau wajitokeze tuweze kuyajadili mambo haya katika siku pekee ya maadhimisho.”
Ofisa Habari wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini, Usia Ledema alisema wanathamini mchango wa vyombo vya habari kwani vimeibua mambo mengi yaliyokuwa yamefichwa.
Alisema pasipokuwa na vyombo vya habari hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana maana vinaimarisha amani ya Taifa husika.
Maadhimisho hayo yatahudhuriwa na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi akiwamo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.

Post a Comment