TUME
ya Maendeleo ya Ushirika inakusudia kuvifuta vyama 1,862 vya ushirika
nchini, kutokana na kukiuka matakwa ya sheria ya vyama hivyo na
kushindwa kutimiza masharti ya usajili wake.
Miongoni
mwa vinavyofutwa ni Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo (Saccos) cha
Madiwani wa Manispaa ya Kinondoni, Saccos ya Shirika la Usafiri Dar es
Salaam (UDA), Madiwani Saccos ya Kagera na cha Madiwani wa Mpwapwa na
vingine vya ushirika.
Akizungumza
na wanahabari juu ya kusudio hilo, Kaimu Mrajisi wa vyama hivyo na
Mtendaji Mkuu wa Tume hiyo, Dk Audax Rutabanzibwa alisema hatua
watakazochukua baada ya kufuta vyama hivyo ni kuendelea kuwafuatilia
waliosajili vyama hivyo na warajisi wasaidizi ili kubaini ukweli wa
uanzishwaji wake.
Alisema kuna uwezekano waliosajili walishirikiana na warajisi wasaidizi ili kuanzisha vyama hewa kwa lengo la kujipatia fedha.
Alitaja
vyama vitakavyofutwa kulingana na maeneo, kwa upande wa Arusha kuwa ni
83, Dar es Salaam 91, Dodoma 50, Geita 16, Iringa 74, Kagera 240, Katavi
19, Kigoma 38, Manyara 73, Mara 203, Morogoro 278, Mtwara 52, Njombe
18, Pwani 324, Rukwa 14, Ruvuma 14, Shinyanga 89, Simiyu 93, Singida 15,
Tanga 77 na Lindi kimoja.
Aliongeza
kuwa kutokana na sababu hizo, vyama vinavyokusudiwa kufutwa ni 1,862 na
vitafutwa baada ya siku 90 kuanzia Mei 13, mwaka huu.
|
Post a Comment