Bunge la Ujerumani limepitisha muswada wa kuziweka nchi za Algeria,
Morocco na Tunisia, katika orodha ya mataifa ambayo ni salama, hatua
ambayo inalenga kupunguza idadi ya watu wanaoomba hifadhi nchini
Ujerumani.
Kwa ujumla, wabunge 422 wa bunge la Ujerumani, wamepiga kura kuonyesha
kukubaliana na muswada huo wa kuziainisha nchi hizo tatu zilizopo
Kaskazini mwa Afrika kuwa ni salama. Kulikuwa na kura 143 za kupinga
mabadiliko hayo ya sheria, wakati wabunge watatu hawakupiga kura zao.
Hatua hiyo itaifanya serikali ya Ujerumani sasa kuongeza juhudi kwenye
utaratibu wa kuwarejesha makwao Waalgeria, Wamorocco na Watunisia
waliokuwa wakiomba hifadhi nchini Ujerumani.
Hata hivyo, maamuzi haya yanatakiwa kuridhiwa na baraza la juu la bunge
la Ujerumani, Bundesrat, kabla ya kuanza kwa utekelezaji wake. Chini ya
sheria ya Ujerumani, wakimbizi wanaotoka katika nchi ambazo
zinatambulika kuwa ni salama, hawana haki ya kuomba hifadhi.
Hata hivyo, muswaada huu unaendelea kupingwa vikali na baadhi ya vyama
vya siasa na wanaharakati wanaopigania haki za wahamiaji. Miongoni mwao
ni Chama cha Kijani. "Hali ya haki za binadamu katika nchi hizo
zinazoitwa kuwa ni salama si shwari", mtaalamu wa masuala ya nje wa
chama hicho Jürgen Tritin ameliambia gazeti la Ujerumani la Saarbrücker
Zeitung.
Takriban watu 26,000 kutoka nchi hizo waliomba hifadhi mnamo mwaka 2015
Ndani ya bunge hilo, Trittin aliendesha kampeni ya kuwataka wawakilishi
wa majimbo ya Ujerumani chini ya chama hicho kupiga kura ya kupinga
mabadiliko yaliyomo katika muswada huo, utakapowasilishwa tawi la juu la
Bunge, linalokuwa na uwakilishi wa serikali.
Serikali ya mseto ya vyama vya Kijani na CDU, inayoongoza jimbo la
Baden-Württemberg lililoko Kusini mwa Ujerumani, imeahidi kupiga kura ya
kuiunga mkono kanuni hiyo mpya, iwapo tu hakutakuwepo na vikwazo vya
kikatiba.
Mwaka 2014, jimbo hilo lililokuwa likiongozwa na serikali ya
mseto ya chama cha kijamii cha SPD na Chama cha Kijani, pia liliunga
mkono mpango wa Ujerumani wa kuongeza nchi ambazo ni salama, ambao
uliruhusu Serbia, Macedonia na Bosnia na Herzegovina, kuongezwa katika
orodha. Uamuzi huo pia ulikumbana na vipingamizi vikali kutoka chama cha
Kijani.
Viongozi wa taasisi mbalimbali kubwa za kijamii nao pia wameeleza
wasiwasi wao juu ya dhamana ya wanaoomba hifadhi kwa kusema kwamba
utaratibu wake unaweza kudhoofishwa na kanuni hiyo.
Huku akiutetea muswada huo, waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani,
Thomas de Maiziere, amewaondoa wasiwasi, na kusema Ujerumani itaendelea
kushughulika na masuala ya kibinadamu.
Kwa kuzingatia idadi kubwa ya wakimbizi Barani Ulaya, Ujerumani imekuwa
ikipata ukusoaji mkubwa katika miezi ya hivi karibuni wa kupunguza idadi
ya watu wanaoomba hifadhi. Mwaka jana, Ujerumani ilishuhudia kuingia
kwa kiasi ya wakimbizi Milioni 1.1, wengi wao wakitokea Syria na
Afghanistan.
Post a Comment