0

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameelezea kufurahishwa na utoaji wa huduma za afya kwa wazee katika hospitali mbalimbali alizotembelea na kukuta yameanzishwa madirisha maalum ya kuhudumia.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Viongozi wa Mtandao wa Wazee waliomtembelea ofisini kwake mjini Dodoma.

Akizungumzia kuhusu suala la wazee kupewa elimu ya mapambano dhidi ya UKIMWI aliwataka waandaaji wa matamasha na semina za mafunzo hayo kujumuisha watu wote wakiwemo wazee.

Naye Mwenyekiti wa mtandao huo , Bw. Sebastian Bulegi alisema lengo la kumtembelea Waziri Mkuu ni kumuomba awafikishie shukurani zao kwa Rais Dk Magufuli kwa kuwapatia wizara maalumu inayoshughulikia masuala yao.

“Vile vile shukurani hizi tufikishie kwa mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli kwa kufanya wazee kuwa agenda yake ya kwanza na tayari ameshatembelea makazi ya Nunge Kigamboni (Dar es Salaam) na Bukumbi (Mwanza),”alisema.

Mwenyekiti huyo ambaye aliambatana na wajumbe wanane wa mtandao huo unaoundwa na Asasi 26 za wazee katika ngazi za wilaya na mkoa kutoka mikoa ya Kigoma, Tanga, Arusha, Mwanza, Lindi na Dodoma, aliiomba Serikali isimamie kutokomeza mauaji ya wazee.

Ombi lingine alilolitoa kwa Serikali ni utekelezwaji wa Sera ya Wazee ya mwaka 2003, Sera ya Matibabu bure kwa wazee, mafunzo ya kupambana na UKIMWI pamoja na uwakilishi katika ngazi za kutoa maamuzi.

Pia wazee hao wamemhakikishia Waziri Mkuu kwamba wamekubali ombi linalotolewa na viongozi wakuu wa nchi la kuwataka wawaombee ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo, baada ya kuridhishwa na utendaji kazi wa Serikali.

Post a Comment

 
Top