0


Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe.
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imepokea ushauri uliotolewa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT- Wazalendo) wa kuishitaki Benki ya Standard (ICBC) ya Uingereza, kuhusu ufisadi uliofanyika katika mkopo wa Dola za Marekani milioni 600 (Sh trilioni 1.2) ambazo Serikali ilikopa kwa kutumia hati fungani.

Ushauri mwingine uliotolewa na Zitto ambao Waziri Mkuu amesema Serikali itaufanyia kazi ni kuhusu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuwafikisha mahakamani wahusika wa sakata la akaunti ya Tegeta Escrow, ili sheria ichukue mkondo wake.
Zitto alitoa ushauri huo bungeni mjini hapa juzi, wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, iliyowasilishwa na Waziri Angela Kairuki.
Hotuba ya bajeti ya ofisi hiyo inajadiliwa na wabunge pamoja na ile ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), iliyowasilishwa na Waziri wake, George Simbachawene.
Akizungumza na wanahabari jana, Waziri Mkuu alisema, hoja ya Zitto ina mashiko na akiwa msimamizi wa shughuli za Serikali bungeni, atahakikisha ushauri huo unafanyiwa kazi. “Sisi kama Serikali tutaifanyia kazi na pale tutakapoona tumefikia katika hatua ya kutoa taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa ushauri huo, tutafanya hivyo,” alisema.
Benki ya Standard Kuhusu Benki ya Standard ya Uingereza, Zitto alisema mkopo huo wenye riba yenye kuweza kupanda na kushuka, umeanza kulipwa Machi mwaka huu na utalipwa mpaka mwaka 2020 kwa mikupuo tisa inayolingana.
Alisema, ifikapo mwaka 2020, Tanzania itakuwa imelipa deni hilo pamoja na riba ambayo ni Dola za Marekani milioni 897 sawa na Sh trilioni 2, huku akidai kuwa mkopo huo umegubikwa na ufisadi na wapo baadhi ya Watanzania wamefikishwa mahakamani kuhusu sehemu ya mkopo huo.
Alisema Takukuru katika kesi hiyo, inasaidiwa na wataalamu kutoka Uingereza katika kesi inayohusu Benki ya Uingereza, huku kukiwa na Watanzania walioandika ‘petition’ kutaka Benki ya Standard kuchunguzwa wakitaka ukweli wote kujulikana.
Escrow Kuhusu IPTL Tegeta Escrow, Zitto alisema mwaka 2014, Takukuru iliijulisha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kwamba ilikuwa inachunguza na kumaliza uchunguzi kuhusu miamala ya kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow Benki Kuu ya Tanzania kwenda Benki ya Stanbc Tanzania.
Alisema katika taarifa zote ambazo Takukuru inatoa kuhusu kesi za ufisadi, hakuna mahali inapozungumzia maendeleo ya suala hilo.

Post a Comment

 
Top