0


Mwanza. Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Nyashana, Kata ya Mbugani Wilaya ya Nyamagana, mkoani hapa, Novert Balilemwa anadaiwa kutoweka na Sh100,000 zilizotolewa na idara ya afya kwa ajili ya kununua chakula cha wanafunzi watakapokuwa wanameza dawa za minyoo na kichocho.

Tukio la mwalimu kutoweka na fedha hizo lilibainika Mei 19, siku ambayo utoaji wa dawa kwa ajili ya kinga ya magonjwa hayo yasiyopewa kipaumbele ulipofanyika.

Akizungumzia tukio hilo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Wandago Robert alisema aliondoka na fedha hizo kwa sababu zisingetosha kununulia chakula cha kuwatosha wanafunzi wote.

“Shule ina jumla ya wanafunzi 1,613, kwa maana hiyo fedha zisingetosha kununua chakula. Tulichofanya ni kuwaagiza wanafunzi kuja na chakula chao kutoka nyumbani,” alisema Robert.

Akizungumzia tuhuma dhidi yake, mwalimu Balilemwa alisema hakununua chakula kama ilivyopangwa kwa sababu alikuwa akisubiri orodha ya wanafunzi wanaohitaji huduma hiyo, baada ya kujua wangapi hawakuja nacho kutoka nyumbani kama walivyoagizwa.

“Kabla sijafanikiwa kujua idadi kamili ili niende kununua chakula kwa kutumia fedha zilizotolewa na Serikali, ndipo wakaguzi wa zoezi la kunywesha dawa walipowasili na kulalamikiwa na watoto kuwa hawajapewa chakula,” alisema.

Ofisa Elimu wa Wilaya ya Nyamagana, Cloude Bulle alisema mwalimu huyo alifanya kosa na kwamba, alipaswa kutoa taarifa ofisini kwake kama fedha hizo zisingetosha kununua chakula.

Post a Comment

 
Top