0


Kiteto. Mkazi wa Kijiji cha Ngapepa Kata ya Kijungu wilayani Kiteto Mkoa wa Manyara amenusurika kifo baada ya kuchomwa kisu tumboni na mtu asiyefahamika wakati wakimgombea mwanamke.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Francis Massawe alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea juzi usiku.

Alisema polisi wanamshikilia mwanamke anayedaiwa kuwa chanzo cha ugomvi huo, mkazi wa Kijiji cha Ngapepa ili aisaidie kumtambua mtuhumiwa aliyetoroka.

Alisema chanzo cha tukio hilo inadaiwa ni wivu wa mapenzi uliosababishwa na mwanamke huyo kutembea na wanaume wawili kwa wakati mmoja.

“Uchunguzi wa awali unaonyesha watu hawa hawafahamiani na wala hakuna ambaye ni mume wa mwanamke huyo na anayewafahamu ni mwanamke aliyesababisha ugomvi,” alidai Massawe.

Alisema majeruhi huyo amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kiteto akipatiwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri.

Hata hivyo, Kamanda Massawe alishauri jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi hasa katika masuala ya mapenzi na kuhamaki bila kujua historia ya mahusiano yoyote kwani wanasababisha matukio ambayo baadaye huja kuyajutia.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, Mariam Abdalah na Julius Lucas walidai kitenda hicho kilichangiwa pia na ulevi.

Post a Comment

 
Top