0


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiiano Profesa Makame Mbarawa amesema Serikali haitaongeza muda katika zoezi zima la uzimaji wa simu feki ifikapo Juni 16 mwaka huu.

Amesema serikali imeamua kuchukua uamuzi huo kutokana na madhara mbalimbali yatokanayo na simu hizo ikiwemo ya kiafya na kusisitiza kuwa serikali inapoteza mapato mengi kutokana na uingizwaji wa simu hizo nchini.

Aidha, Profesa Mbarawa ameongeza kuwa kwa sasa jopo la wataalam kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) limepelekwa mkoani Singida kwa ajili ya kutoa elimu ya utambuzi wa simu hizo ili kuweza kuwasaidia wananchi kubaini kwa urahisi.

Amesisitiza wananchi kuchukua tahadhari kabla ya kununua simu ikiwemo kumuuliza muuzaji kabla ya kununua, kudai risiti na kuituinza ili kudhibiti uingizwaji na usambazaji wa bidhaa hizo nchini.
Katika hatua nyingine, Waziri Mbarawa amesema kuwa suala la mkongo wa taifa linaendelea vizuri ambapo serikali kwa kushirikiana na watoa huduma wa mawasiliano wanaendelea na usimikaji wa minara ya mawasiliano katika sehemu mbalimbali za nchi hususan vijijini ili kuleta huduma bora za mawasiliano nchini.

Ameongeza kuwa uwepo wa mkongo huo nchini kumepelekea mapinduzi katika sekta ya mawasiliano, mabenki na kuiongezea Serikali pato kwani hata nchi za jirani hutumia mkongo huo katika kupata mawasiliano yaliyo bora.

Tathmini imebainisha kuwa kutokana na uwepo wa mkongo huo nchini watumiaji wa simu wamefikia milioni 39.7 na wa intaneti kufukia milioni 17.

Post a Comment

 
Top